Sunday, April 29, 2012

Kiama cha Mawaziri

WAKATI mawaziri wanaounda Serikali ya Awamu ya Nne wakiendelea kupata usingizi wa mang’amung’amu kwa hofu ya kupanguliwa, kuna taarifa kwamba idadi kubwa ya mawaziri wa zamani wataachwa na sura mpya hususan vijana kutawala baraza jipya.

Joto la mabadiliko ya Baraza la Mawaziri limeshika kasi baada ya Kikao cha Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyokutana juzi jijini Dar es Salaam juzi na kuridhia mapendekezo ya Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa chama hicho, kuwataka mawaziri wanaoandamwa na kashfa mbalimbali katika wizara zao, kuachia ngazi.

Taarifa ya Rais Kikwete kutaka kusuka upya Baraza la Mawaziri ilitangazwa juzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alipokutana na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizikia kwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya CCM.

Vyanzo vya gazeti hili vimeeleza kuwa mbali na Rais kutumia kigezo cha udhaifu uliobainishwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), atawaengua pia wale wanaoshindwa kuwajibika na wale wenye kasi ndogo ya uongozi.

Mawaziri wanaotuhumiwa kushindwa kuwajibika, wengi wao ni vijana hivyo huenda akachagua vijana wenzao kuchukua nafasi zao.

Habari hizo zinaeleeza kuna uwezekano mkubwa katika mabadiliko hayo, mawaziri wazee na wagonjwa wakakumbwa na fagio hilo.

Vijana wanaotajwa kuwa huenda wakaingia katika Baraza jipya la Mawaziri ni pamoja na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba, Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, Mbunge wa Handeni, Dk Abdallah Kigoda, Mbunge Kahama, James Lembeli, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango na Mbunge wa Igunga Dk Dalaly Peter Kafumu.

Mwingine anayetajwa kuingia katika baraza hilo ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha Rozi Migiro ambaye anatarajiwa kurejea nchini hivi karibuni baada ya kumaliza mkataba wake wa kuutumikia umoja huo.

Hata hivyo baadhi ya wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema huenda, Rais Kikwete akalipunguza kwa kiasi kikubwa baraza hilo kwa kuvunja na kuunganisha baadhi ya wizara kama moja ya njia za kubana matumizi, jambo linaloonekana kuwa ni moja ya matatizo makubwa yanayoikabili Serikali yake.

Baraza lililopo sasa lina mawaziri 30 na manaibu mawaziri 21 ambao kwa pamoja wanafikia 51

Alipokuwa akiingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Rais Kikwete aliunda baraza ambalo lilikuwa na mawaziri 60, lakini baadaye alilivunja na kupunguza idadi hiyo.

Tatizo ni mfumo sio mawaziri

Wasomi nchini wamesema hata kama Baraza la Mawaziri litabadilishwa Tanzania bado itaendelea kuwa nchi inayotisha katika ubadhilifu wa mali za umma na kwamba suluhisho pekee ni kubadili mfumo mzima wa utawala.

Wakati wasomi hao wakieleza hayo, Edwin Mtei ambaye alikuwa Gavana wa kwanza mzalendo wa Benki Kuu Tanzania (BoT) na Waziri wa Fedha, alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwa na maamuzi magumu ya kuwatimua kazi viongozi wenye tuhuma mbalimbali kama ilivyokuwa kwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.

Mtei alisema kuwa wakati akiwa Waziri wa Fedha na Mipango alitofautiana na Mwalimu Nyerere kuhusu kupunguza thamani ya Shilingi na kuamua kumwandikia barua ya kujiuzulu wadhifa wake.

“Nilipomwandika barua hiyo na yeye akanieleza wazi kuwa hawezi kukubaliana na wazo langu, nikaamua kuacha uwaziri kwa amani, hivi hawa mawaziri wa sasa wanashindwa nini?” alihoji Mtei.

Alisema tatizo la Rais Kikwete ni kuwa mzito wa kuchukua maamuzi na kuongeza; “Anasitasita sana kuwawajibisha watu wazembe”.

Mtei ambaye pia ni muasisi wa Chadema, alidai kuwa mbali na Rais Kikwete kusita kutoa maamuzi, pia hatekelezi yale ambayo yamewafanya wananchi wakamchagua ikiwa ni pamoja na kuwafumbia macho viongozi wanaotafuna kodi za wananchi.

“Nilifanya kazi Mwalimu Nyerere, alikuwa kiongozi ambaye hasiti kuwachukulia hatua viongozi waliokuwa wakimwangusha katika utendaji wake,” alifahamisha Mtei

Juzi Rais Kikwete alisikia kilio cha wabunge, vyama vya siasa, wananchi wa kawaida na wanaharakati kutaka mawaziri waliohusishwa na kashfa kwenye ripoti ya CAG wajiuzulu na kukubali kulisuka upya Baraza lake la Mawaziri.

Mawaziri waliotajwa katika ripoti ya CAG na kushinikizwa kujiuzulu ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali  za Mitaa(Tamisemi), George Mkuchika.

Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala aliliambia gazeti hili jana kuwa kubadilishwa kwa baraza hilo hakuwezi kuondoa ufisadi na kwamba, tatizo linaloikabili nchi ni mfumo mzima wa utawala ambao umejaa ubadhilifu mkubwa.

Alisema, viongozi nchini wanatakiwa kujenga utamaduni wa kuwajibika na kusisitiza hali hiyo pekee ndio itakiondoa chama tawala katika utamaduni wa kulindana ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo chanzo cha kukithiri kwa ufisadi.

“Naipongeza Serikali kwa hatua inayotaka kuifanya ila waliotuhumiwa walitakiwa kuachia ngazi baada ya kushutumiwa na wabunge na sio kusubiri mpaka kuwajibishwa kwa lazima,” alisema Profesa Mpangala.

Aliongeza kuwa tatizo lililopo hivi sasa ni rushwa kuota mizizi katika ulingo wa siasa jambo ambalo linawafanya viongozi wengi wanaochaguliwa, kujikita katika vitendo hivyo na ubadhilifu wa mali ya umma kwa kuwa huingia madarakani kwa kutumia fedha.

“Watu siku hizi wanatumia mamilioni katika chaguzi, mtu wa namna hii akishinda kwanza ni lazima arudishe gharama alizotumia, tusipoondoa rushwa hii katika siasa kila sekta nchini itakuwa haitamaniki kwa ufisadi,” alisema Profesa Mpangala.

Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk Kitila Mkumbo, alisema kuwa kubadilishwa kwa baraza hilo hakuwezi kusaidia chochote kwa kuwa mfumo wa utawala ndio wenye matatizo.

“Kinachotakiwa ni kubadilishwa kwa mfumo wa utawala ambao umeshamiri rushwa. Binafsi naona kuwa kubadili baraza la mawaziri ni sawa na kupita njia ya mkato, hapa kikubwa ni kutengeneza mfumo wa uwajibikaji,” alisema Dk Mkumbo na kuongeza kuwa hatashangaa kuona mawaziri wapya nao wakifanya yale yale ambayo yanataka kuwaondoa wenzao.

Naye Profesa Abdallah Safari alisema kuwa, kubadilishwa kwa baraza hilo sio mara ya kwanza na kwamba huenda Rais Kikwete anataka kulibadili baraza hilo ili kuonyesha kuwa amechukizwa na waliyoyafanya mawaziri wake.

“Labda anawapa moyo tu watu, binafsi naona Rais Kikwete ndio mwenye matatizo kwa kuwa katika utawala wake hii itakuwa mara ya pili kubadili Baraza lake la  Mawaziri,”  alisema Profesa Safari.

Alidai kuwa Rais Kikwete amekuwa mtu wa kuwabeba watu wake wa karibu na kwamba, huenda hali hiyo imechangia kutokea ubadhilifu katika utawala wake.

“Naona kama Political game (mchezo wa kisiasa), Rais anaonekana kuwa amekasirishwa lakini mwisho wa siku, yeye ndio anaonekana kuwa na tatizo,” alisema Prof. Safari.

Kutoka ndani ya Kamati Kuu CCM


Suala la kujiuzulu mawaziri waliotajwa katika ripoti ya CAG, juzi lilitawala Kikao cha Kamati Kuu ya CCM, huku Waziri Mkuu Mizengo Pinda akielezea jinsi baadhi ya mawaziri wanavyoitafuna nchi.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho, zinaeleza kuwa Pinda alitikisa mkutano huo alipowasilisha Ripoti ya Utendaji Kazi wa Serikali bungeni na yaliyojiri bungeni wakati wabunge walipotaka mawaziri nane kujiuzulu na uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki.

Chanzo chetu cha habari kutona ndani ya kikao hichi kimeeleza kuwa, Pinda alisema mawaziri watano waliokubali kuandika barua ya kujiuzulu baada ya kupata shinikizo la kikao cha faragha cha wabunge wa CCM na wengine hawakufanya hivyo.

Chanzo chetu kilieleza kuwa Pinda aliwataja mawaziri waliowasilisha barua za kujiuzulu kuwa ni Waziri wa Kilimo na Chakula, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda.

Alisema Waziri Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, hawakuwasilisha barua zao huku wakitoa sababu za kushindwa kufanya hivyo.

Mawaziri hao wanane katika utetezi wao walioutoa kwenye kikao cha faragha cha wabunge wa CCM, Dk Chami alisema hakufanya hivyo kwa sababu kujiuzulu kwake kunaweza kuleta matatizo kwa chama kwani kama atamua kuachia ngazi na ubunge, ni wazi wapinzani watachukua jimbo la Moshi Vijijini.

Waziri Nundu inaelezwa kuwa alijitetea akisema hawezi kujiuzulu kwa sababu haoni makosa ambayo ameyafanya, huku Waziri Mkulo akishindwa kuandika barua hiyo kwa vile alikuwa nje ya nchi kikazi.

Kwa upande wa mawaziri walioandika barua, Waziri Ngeleja alisema alindika barua ya kujiuzulu ingawa hana hatia binafsi katika tuhuma zilizoko kwenye ripoti ya CAG, huku Waziri Maige akieleza kuwa hata yeye hana hatia binafsi kuhusiana na tuhuma zilizoikumba wizara yake.

Katika utetezi wake Waziri Maghembe alisema pamoja kuwa amekubali kujiuzulu, lakini hana hatia, kilichosababisha wizara yake kuchelewa kupatikana kwa mbolea ya ruzuku kwa wakulima ni benki kuchelewa kutoa udhamini wa mkopo.

Alisema badala ya benki kutoa udhamini huo Januari, ilitoa Machi, hali ambayo ilisababisha kuchelewa wakulima kupata pembejeo kwa wakati unaofaa.

Mawaziri, Dk Mponda na Mkuchika walikubali kujiuzulu bila kutoa utetezi.


Chanzo chetu kinaeleza kuwa Pinda alisema baadhi ya mawaziri wamepoteza hadhi na heshima ya kuendelea kuwa katika nafasi hizo kutokana na kufanya mambo yasiyofaa mbele ya jamii.

Alitoa mfano wa waziri mmoja (jina tunalo) ambaye hivi sasa madalali wanaposikia nyumba inauzwa jijini Dar es Salaam, wanamtafuta wakiamini ana uwezo wa kununua.

Pinda alieleza kukerwa na mawaziri wanaoendelea kulumbana kupitia vyombo vya habari kuhusu madudu ambayo yameripotiwa na CAG katika wizara zao, kuwa hali hiyo haifai kuendelea kutokea.

Malumbano ya mawaziri

Mawaziri ambao wameripotiwa kutupiana lawama kuhusu uozo uliozikumba wizara zao ni, Waziri wa Uchukuzi, Nundu na Naibu wake Athuman Mfutakamba, Waziri Chami na Naibu wake Lazaro Nyalandu.

Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu katika utetezi wake alisema naibu wake, Athuman Mfutakamba) amekuwa akishinikiza Kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC),ipewe kazi ya kujenga gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ilimgharamia safari kadhaa kwenda nje.

Waziri Nundu pia alishangazwa na shinikizo la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wake, Peter Serukamba kuingia na kushinikiza CCCC ipewe kazi hiyo akahoji kuna nini?

Hata hivyo, naibu wake, Mfutakamba alipoulizwa kuhusu safari zake hizo za nje kugharamiwa na CCCC na baadaye kuandika ripoti akishinikiza ipewe kazi ya kujenga gati hizo, alikiri kusafirishwa na kampuni hiyo, lakini akasema alifuata taratibu zote za kiserikali.

Wakati Nundu na naibu wake wakilipuana, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazoro Nyalandu naye alionekana kutua mzigo wa kashfa ulioigubika wizara hiyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege akisema alimshauri waziri wake, Dk Chami kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo mapema.

Kwa upande wake Dk Chami alisema hadi Bunge linamalizika mjini Dodoma wiki hii, alikuwa hajaiona ripoti ya kamati ndogo ya Bunge iliyomchunguza Ekelege ambayo ingemsaidia kupata tuhuma zinazomkabili mkurugenzi huyo ili kuchukua hatua.

Mbali ya hoja hiyo ya mawaziri kujiuzulu, Pinda pia aliwasilisha taarifa ya uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mshariki uliofanyika katika kikao cha Bunge kilichomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma.

Katika ripoti hiyo inaelezwa Waziri Mkuu alimwanika hadharani kigogo mmoja wa CCM kuwa alishiriki kuvurugua uchaguzi huo baada ya ‘kuigiza mkono’ wake hadi kusababisha kura kurudiwa kuhesabiwa.

Alisema kigogo huyo ambaye alikuwa akimpigia debe mgombea mmoja kutoka chama hicho, aliingia katika mchakato wa kuhesabu kura ili mgombea aliyemtaka apite.

Hoja hiyo ikaibua hamaki kwa baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ambao walitaka suala hilo lijadiliwe katika kikao hicho ambacho kigogo huyo ni mjumbe pia.

Hata hivyo, busara za Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Kikwete na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Wiliam Lukuvi zilisaidia kumnusuru kigogo huyo.

Taarifa zinaeleza kuwa Rais Kikwete aliwaambia wajumbe wa Kamati Kuu kuwa suala hilo halikuwa ajenda ya kikao hicho na kwamba suala lilokuwa mezani ni la mawaziri wanaotuhumiwa kushindwa kuwajibika kujiuzulu.

Baada ya Pinda kuwasilisha ripoti hiyo, Rais Kikwete alisema atawaondoa mawaziri wote ambao wizara zao zimetajwa katika Ripoti ya CAG kujaa ufisadi.

Vile vile, alienda mbali zaidi na kueleza kuwa hataishia katika kuwaondoa mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi tu, bali atawaondoa na mawaziri ambao wana kasi ndogo ya utendaji wa kazi.

Kwa upande wa viongozi wa mashirika ya umma wanaotuhumiwa kwa ufisadfi, Rais Kikwete alisema atawaondoa wote waliotajwa katika ripoti ya CAG na atazivunja bodi za wakurugenzi wa mashirika hayo.

Rais Kikwete pia alisema kuwa atatangaza wakuu wapya wa wilaya katika wilaya mpya ambazo hazijapata viongozi wake hivi karibuni.



Mwananchi Newspaper

No comments:

Post a Comment