RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete sasa anajipanga
kuunda Baraza jipya la Mawaziri baada ya yeye kuwasilisha hoja ya
kulivunja baraza hilo kwenye Kamati Kuu ya CCM leo na kamati hiyo
kuridhia hoja yake. Rais Kikwete analazimika kufanya hivyo baada ya
mawaziri waliotuhumiwa kufuja fedha za umma bungeni hivi karibuni kugoma
kujiuzulu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo na CCM
baada ya kikao cha Kamati Kuu, Rais Kikwete amewasilisha wazo la
kulivunja Baraza lake la Mawaziri na kulisuka upya ili kuwaondoa
viongozi walioshindwa kusimamia wizara zao.
“Kamati Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais Kulisuka Upya Baraza lake la Mawaziri
na taasisi zingine zilizoanishwa katika ripoti hizo. Imesisitiza
utekelezaji wa uamuzi huo ufanywe mapema iwezekanavyo,” imesema taarifa
hiyo.
Kamati Kuu pia imeridhishwa na kuheshimu haki na wajibu wa wabunge
kujadili utendaji wa Serikali yao na kupongeza juhudi za serikali
kuhakikisha kuwa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali inajadiliwa kwa uwazi na hivyo kuibua mapungufu yaliyojadiliwa.
Aidha taarifa hizo zote zimewasilishwa kwenye kikao cha Kamati Kuu na
kujadiliwa. Pamoja na taarifa hizo Kamati Kuu imepokea taarifa ya jinsi
Rais alivyojipanga kuchukua hatua za kuwawajibisha mawaziri na
watendaji wa serikali na wale wa mashirika ya umma waliobainika kuhusika
na ubadhirifu ulioinishwa na taarifa ya Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa
hesabu za Serikali, Kamati za kudumu za bunge na wabunge bungeni.
katika kikao hicho pia kilipokea taarifa na maazimio ya Kamati ya
wabunge wa CCM na Kamati ya uongozi ya wabunge wa CCM juu ya
kilichotokea kwenye bunge lililopita mjini Dodoma.
Aidha Kamati Kuu imeipongeza Kamati Teule ya baraza la wawakilishi
Zanzibar iliyoundwa kuchunguza utendaji katika sekta mbalimbali kwenye
serikali ya mapinduzi Zanzibar kwa taarifa yao.
Kamati Kuu inawapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa jinsi
walivyojadili taarifa hiyo na pia Kamati Kuu inaipongeza Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kwa kuipokea taarifa na kuanza kuifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment