Imeandikwa na: Staphord Kwanama
Wapendwa wasomaji ni wiki nyingine tena kama
ada tuanze kwa kumshukuru Mungu kutujalia uhai. Napenda kutumia fursa
hii kuwashawishi baadhi ya watu wanaofikiria kuanzisha biashara.
Bila
shaka endapo msomaji anafanya biashara atakuwa amepata mambo matatu
ambayo yatakusaidia kurekebisha mahali ambako ulikosea.
Je, ni njia zipi unapaswa kupitia ili kuwa mjasiriamali? Hili ni swali gumu sana kwa sababu majibu yanatofautiana.
Kama
hujawahi kufikiria kuwa mjasiriamali na inatokea bahati mbaya unatafuta
kazi, lakini hujapata na ukaamua kuanzisha biashara utakuwa katika
wakati mgumu kupata mafanikio.
Lakini kwa mtu mwingine ambaye
amekuwa akifikiria kuwa mjasiriamali, hakika ukianza biashara utakuwa
katika nafasi nzuri ya kufanikiwa.
Zifuatazo ni mbinu za kuwa mjasiriamali bora:
1.
Elimu: Pata taarifa mbalimbali za ujasiriamali fahamu faida na
changamoto. Pia fahamu tabia za wajasiriamali waliofanikiwa ujenge
taswira ya mjasiriamali wa namna gani utakuwa. Mathalani kama bado uko
shule au chuo hudhuria vipindi vingi vya elimu ya ujasiriamali.
Kama
hauko shule, tafuta namna yoyote upate elimu mfano elimu ya watu
wazima, makongamano, warsha, midahalo, mafunzo, kuangalia televisheni
na sikiliza redio. Angalizo: jipangie muda maalumu ili usitumie muda
mwingi kujifunza na kuchelewa kuanza biashara. Suala la elimu
linaendelea hata baada ya kuanzisha biashara.
2. Jenga ndoto
kubwa: Katika hatua nyingine ili kuwa mjasiriamali bora, weka mikakati
ya kwamba unataka kuwa mjasiriamali wa aina gani. Fikiria miaka mitano,
kumi mpaka 20 itakuaje. Pia fikiria namna gani utaiendesha biashara ya
ndoto yako.
Katika hatua hii usisumbuke kufikiria namna ya kupata
fedha ya kuanzisha biashara. Kama utaanza kuwa na wasiwasi wapi utapata
fedha, pia hutaweza kuanza biashara.
Katika hatua hii, wasiliana
na watu mbalimbali wenye biashara, waulize walianzaje. Pia fikiria
mambo makubwa. Usiwaze kufanya vitu vidogo ambavyo kila mtu anaweza
kufanya.
3. Mipango: Baada ya kujenga ndoto yako, andika mipango
mbalimbali jinsi ya kuanzisha biashara. Mipango hii sio mchanganuo wa
biashara bali andika mambo mbalimbali unayojifunza kutoka kwa
wajasiriamali wenzako na tunza vizuri taarifa hizo.
Kama umenunua
gazeti na kuona habari njema kwako chana kipande na tunza, inapendeza
ukiwa na faili au hata bahasha fulani hivi tunza vipande vya karatasi
unazoandika mambo yako siku moja utaifungua na utagundua una taarifa
nyingi za kukusaidia kuanzisha biashara.
4. Fedha: Vyanzo vya
fedha ni akiba kwa mjasiriamali. Kama umeajiriwa kopa kwa ajili ya
biashara, pia pokea msaada kutoka kwa wazazi, ndugu jamaa au rafiki.
Wakati mwingine unaweza kutafuta wawekezaji kama biashara ni kubwa.
5.
Maandalizi: Baada ya hatua hizo fanya maandalizi, fanya mchanganuo
kujua wateja wako ni nani, wanapenda nini, uwezo wao wa kununua.
Jipange namna gani taarifa zitawafikia endapo utaanzisha biashara.
Biashara ni matangazo. Pia kama utahitaji wafanyakazi, ni muda mwafaka
kuchanganua utaanza na wangapi kwa nafasi zipi. Fikiria zaidi mahitaji
ya biashara unayotarajia kuanzisha kwa mfano leseni, vibali na eneo la
biashara.
6. Anzisha biashara: Baada ya mipango na maandalizi
kukamalika unashauriwa kuanzisha biashara. Tangaza biashara yako,
fanya tafrija fupi, karibisha familia, jamaa na marafiki ili wajue
biashara yako.
Katika tafrija hiyo unaweza kupata wateja au mtandao wa biashara yako. Unaweza kuanzia hapo.
7.
Fanya marekebisho ya mipango: Wahenga walisema mipango sio matumizi kwa
kuwa inawezekana kabisa uliyoyapanga kabla ya kuanza biashara, yakawa
tofauti.
Kutokana na hali hiyo chukua fursa ya kufanya marekebisho haraka iwezekanavyo na kuboresha maeneo yenye mahitaji.
Kwa
msaada zaidi tembelea ‘smallbusinessfinancing.com’. au wasiliana kwa simu namba zifuatazo
0712 066 064
No comments:
Post a Comment