Thursday, July 12, 2012

Dk.Slaa:Siendi Polisi ng'o

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, amesema hatakwenda polisi kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano kwa sababu Jeshi hilo limekuwa na desturi ya kumfanyia mahojiano katika matukio mbalimbali, lakini hawayafanyii kazi.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo kufuatia agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alilotoa kwa Jeshi la Polisi juzi la kuwahoji viongozi wote wa Chadema waliosema wanatishiwa maisha na vyombo vya usalama.

Katibu Mkuu huyo alirejea matukio mbalimbali yaliyotokea kipindi cha nyuma likiwemo lile la Aprili mwaka huu katika uchaguzi mdogo wa kata ya Kirumba, ambapo wabunge wawili wa chama hicho mkoani Mwanza, Highness Kiwia (Ilemela) na Salvatory Machemli (Ukerewe), walivamiwa na kushambuliwa na mapanga na watu waliosadikika kuwa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema jana asubuhi alipokea simu kutoka makao makuu ya jeshi hilo iliyomtaka kufika polisi ili kufanyiwa mahojiano, lakini alisema hayupo tayari kufanyiwa mahojiano mengine mpaka pale watakapofanyia kazi yale ambayo walishawahoji katika kipindi kilichopita.

"Ofisa mmoja wa makao makuu ya polisi alinipigia simu leo asubuhi (jana) akinitaka niende polisi, lakini nimekataa. Siwezi kwenda kwa sababu yapo mahojiano mengi ambayo walinifanyia baada ya matukio kadhaa yaliyohusisha chama chetu kutokea na hawajayafanyia kazi, wayashughulikie hayo kwanza," alisema Dk. Slaa.

Aidha, Dk. Slaa ameitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ukweli wa taarifa ya baadhi ya viongozi wa chama hicho kutishiwa maisha na vyombo vya usalama badala ya kutafuta kujua aliyetoa taarifa hiyo.

“Kazi ya serikali na vyombo vya usalama ni kulinda amani, walichotakiwa kufanya mara tu baada ya kupata taarifa hizi ni kufanya uchunguzi ili kupata ukweli na siyo kutafuta kumjua aliyetoa taarifa hizo,” alisema Slaa.

Alisema taarifa yao ya awali kuhusu kuwindwa kwa viongozi wa Chadema, walisema kuwa wanawatambua baadhi ya maofisa usalama wanaohusika ambao aliwataja kwa majina ya Zoka na Rama na kwamba mmoja kati yao amekuwa akifuatilia nyendo za Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.

Dk. Slaa aliongeza kuwa kamati kuu ya chama hicho imelaani kitendo cha kutaka kudhuriwa kwa viongozi hao na kwamba mpango huo ni wa kuhatarisha amani ya nchi. “Kamati kuu imelaani kitendo cha kutaka kudhuru viongozi wake na imelaani pia mpango wowote uliopo ambao unalenga kuhatarisha amani ya nchi," alisema.

Jumapili iliyopita uongozi wa juu wa Chadema uliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa baadhi ya viongozi waandamizi wa chama chao wanawindwa na watu wanadaiwa kuwa ni usalama wa taifa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freema Mbowe, alisema viongozi hao ni pamoja na Dk. Slaa, Mnyika na aliyekuwa Mbunge wa arusha Mjini, Godbless Lema.

Alisema mipango hiyo inahusisha kuuawa kwa sumu au kuwapelekea majambazi kwa nia ya kuwaua.

OPERESHENI SANGARA II YAIVA

Wakati huo huo, Dk. Slaa ametangaza kuwa chama hicho kinatarajia kuanza mpango wa nchi nzima wa 'Operesheni Sangara' awamu ya pili, kwa lengo la kuimarisha na kujenga chama itakayohusisha mikoa mitano.

Alisema operesheni hiyo itafanyika kwa siku 44 katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Iringa, Singida na Manyara na kwamba vijiji 4,000, kata 806 na majimbo 44 vitafikiwa.



CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment