TUME ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) imesema kipimo cha kupima
ukimwi kwa kutumia mate kitaanza kutumika mwakani kwenye mahospitali.
Kifaa
hicho kilichotengenezwa na wanasayansi wa nchini Marekani kimeelezwa
kuwa na uwezo wa kutoa majibu sahihi kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kati
ya dakika 20 na 40 baada ya kupima.
Imeeleza kuwa kifaa hicho
kinachofahamika kama OraQuick, kimebuniwa sio tu kwa ajili ya matumizi
ya hospitalini bali pia nyumbani na kitaanza kupatikana katika maduka ya
dawa nchini Marekani kuanzia Oktoba mwaka huu kabla ya kusambazwa nchi
mbalimbali duniani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi,
Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Tume hiyo, Beng’i Issa alisema kipimo
hicho kitaanza kwanza kutumika kwenye hospitali na baada ya hapo
wataangalia namna ya kuwaelimisha wananchi ili kiweze kutumika hadi
kwenye ngazi ya jamii.
Mkurugenzi huyo alikuwa akizungumza wakati
wa hafla ya kukabidhi msaada wa gari lililotolewa na Mpango wa
Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) kwenda kwa Umoja wa Mameya na
Viongozi wa Manispaa na Majiji (AMICAALL).
“Ni new development
(maendeleo mapya) ambayo imekuja na serikali imepjipanga kuanzia mwakani
kitaanza kutumika,”alisema Issa.Alisema pia kiwango cha maambukizi ya
ugonjwa huo kimeshuka kwa asilimia 25 wakati kwa vijana kimeshuka kwa
asilimia moja.
Kwa mujibu wa Issa, watu wazima hasa walioko kwenye ndoa ndiyo walioathirika zaidi ikilinganishwa na vijana.
Alisema
pia mwitikio wa watu kwenda kupima ukimwi nao umeongezeka kwa asilimia
40 ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo ilikuwa asilimia
10.“Tunawahamasisha wazazi kuongea na watoto wao na viongozi wa dini
kutusaidia kuwarudisha watu kwenye maadili,”alisema.
Akizungumzia
kuhusu msaada huo, Mwenyekiti wa Amicaall, Amani Mwamwindi alisema gari
hilo litatumika kwa ajili ya kufuatilia shughuli mbalimbali za ukimwi
katika manispaa na majiji.
SOURCE: MWANANCHI NEWS PAPER
No comments:
Post a Comment