Sunday, July 22, 2012

Z'bar kwawaka moto

Kikosi cha Kuzuia ghasia Zanzibar (FFU) jana kimelazimika kutumia maji ya kuwasha na mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI) waliokusanyika katika msikiti wa Mbuyuni kwa lengo lililodaiwa kuwasomea dua waliopoteza maisha katika ajali ya meli ya Skagit.

Mabomu hayo yalianza kupigwa jana majira ya saa 11:30 katika eneo la msikiti wa Mbuyuni ambapo wafuasi wa Uamsho walikuwa wamekusanyika katika msikiti kwa kitambo kirefu.
Barabara nyingi zilifungwa na wafuasi kwa kuweka mawe njiani na kwenye mabanda ya biashara wakayang’oa na kuyatupa barabarani.

Vurugu hizo zimesababisha huduma za usafiri kusimama na Kituo Kikuu cha daladala hakikuwa na gari hata moja na kuathiri mamia ya wananchi wakiwemo wanafunzi. 

Watu wazima na watoto walionekana wakikimbia ovyo na wengine kujisalimisha katika nyumba za watu wakikimbia kishindo cha mabomu na moshi wa mabomu uliyochaganyika na maji ya kuwasha.

Mfanyabiashara katika Soko Kuu la Darajani, Makame Tah, alisema kwamba waliamua kufunga soko kutokana na mabomu yaliyokuwa yakipigwa kuathiri kwa kiwango kikubwa wafanyabiashara katika soko hilo na kupotea kwa hali ya usalama kwa wakati huo.

“Nipo njiani nakwenda nyumbani Amani magogoni kwa mguu hakuna huduma za usafiri na soko kuu limefungwa kutokana na vurugu zilizotokea," alisema Makame.

Katibu wa Jumuiya ya Uamsho na mihadhara ya Kiislamu, Abdalla Said, alisema kwamba wafuasi wa jumuiya hiyo walikusanyika katika msikiti huo kwa lengo la kuwasomea dua watu waliopoteza maisha katika ajali ya meli Zanzibar. 

Alisema kwamba wafuasi hao walianza kukusanyika majira ya saa sita na kusali sala ya Ijumaa na Alasiri kabla ya kuendelea na dua maalum ya kuwaombea watu walikufa katika ajali hiyo.
Hata hivyo alisema kwamba wakati kiongozi mkuu wa JUMIKI, Amiri Farid Hadi, akiongoza kisomo huku wafuasi wake wakiwa wamezunguka msikiti huo, askari wa kikaosi cha kutuliza ghasia walianza kupiga mabomu kutawanya kundi la wafuasi hao.

Uamsho wamekuwa wakifanya kampeni za kutaka Zanzibar kujitenga katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar huku wakiungwa mkono na baadhi ya viongozi wa chama na serikali Zanzibar.

Kabla ya kutokea vurugu hizo usiku wa kuamkia jana kumesabazwa vipeperushi vilivyotengenezwa kwa gharama kubwa  vyenye ujumbe wa kupinga Muungano wa  Tanganyika na Zanzibar.

Vipeperushi hivyo vikiwa na picha za karafuu, matunda aina ya shokshok na doriani vimepambwa na rangi nyekundu na kijani “Koti likikubana livue” Abeid Amani Karume “ Zanzibar tuachiwe tupumue”  na “B Proud B Zanzibar @ tuachiwe tupimue.com vipeperushi ambavyo vimekuwa vikitupwa katika mikusanyiko ya huduma za jamii Zanzibar.

Hata hivyo,  hadi tunakwenda mitamboni, juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Azizi Juma, kuzungumzia chanzo cha vurugu hizo hazikufanikiwa kutokana na simu ya kiganjani kutopokelewa.

Makundi ya watalii walionekana wakikimbia vishindo vya mabomu katika mitaa ya Darajani na Mkunazini Zanzibar.

Mei 26, mwaka kulitokea vurugu kubwa na kusababisha makanisa na baa kuchomwa moto baada ya wafuasi wa Uamsho kufanya jaribio la kutaka kuvamia kituo cha polisi mkoa wa mjini Magharibi kumkomboa Kiongozi wao Sheikh Mussa Juma Issa aliyekuwa akishikiliwa na jeshi hilo.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment