Wednesday, August 8, 2012

Lowassa: Tuko tayari kwa vita



KAMATI ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, imesema majeshi ya Tanzania yapo tayari kiakili na kivifaa ikibidi kuingia vitani kutokana na mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Edward Lowassa alipozungumza na waandishi na habari na kusisitiza Tanzania inaomba isifike katika hatua hiyo, lakini ikibidi wanajeshi wetu wapo imara kutetea mipaka ya nchi hadi tone lao la mwisho la damu.

“Jeshi letu lipo tayari, na tumeridhika na utayari wao na ‘commitment’ yao. Sisi ni moja ya jeshi lililojiandaa vizuri sana na miongoni mwa majeshi mazuri duniani. Tunajivunia vijana wa Tanzania waliopo kwenye jeshi letu. Tupo imara kiakili, vifaa vya kisasa,” alisema.

Alisema kamati hiyo inaunga mkono kauli ya serikali iliyotolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, kwani ni sahihi inayoelezea msimamo wa Tanzania kuhusu jambo hilo.

Alisema kuwa wanategemea jambo hilo litamalizika kidiplomasia ndani kwa ndani ama ikibidi kuomba msaada wa watu wengine kusuluhisha kwa kuwa Tanzania na Malawi ni marafiki na ndugu.

“Watu waliopo mipakani ni ndugu, tusingependa kufika mahali kutokuelewana mpaka kuhusisha vyombo vya ulinzi na usalama, lakini kwa faida ya Watanzania tumepewa maelezo ya jeshi letu, tumeridhika kwamba ikibidi jeshi letu limejipanga vizuri sana.

“Watanzania wasiwe na shaka yoyote, wanajeshi wamejipanga vizuri na kwa uhakika na kama ilivyo ahadi yao, wapo tayari kulinda nchi yetu mpaka tone la mwisho la damu yao,” alisema na kuongeza kuwa kama wabunge, nao wameridhika na maandalizi ya jeshi, kwani wapo imara na timamu.

Alisema serikali haitaki kufika huko, kwani wakati wa Vita ya Uganda mwaka 1978, wananchi waliumia na kwamba kama nchi, inafahamu athari za vita kiuchumi na kwa maisha ya binadamu.

“Hatutaki kufika huko kwani si jambo jema, ndiyo maana tunasema tumalize kwa njia ya mashirikiano na kwa mazungumzo ya kidiplomasia ya mawaziri wanaohusika ikishindikana tutafute msuluhishi,” alisema.

Mwaka 1978, Tanzania iliwahi kuingia katika vita na Uganda, baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Iddi Amin Dada, kuvamia sehemu ya Tanzania na kudai kuwa ni yao.

Juzi, Membe alitoa tamko la serikali na kuyataka makampuni yote yanayoendelea kufanya utafiti wa mafuta katika ziwa hilo kuondoka mara moja pamoja na Serikali ya Malawi kuheshimu mazungumzo yaliyofikiwa. Alisisitiza eneo linalobishaniwa katika ziwa hilo lipo Tanzania.

Alisema pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuzipiga marufuku ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano zilitua katika eneo la Ziwa Nyasa.

“Serikali ya Tanzania inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea na shughuli za utafiti katika eneo hilo zisitishe mara moja kuanzia leo Jumatatu,” alisema Membe na kuongeza kuwa, Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote.

Alisema kwa kuzingatia nyaraka zilizotengenezwa na wakoloni wa Kiingereza mwaka 1928 na 1938, zinaonesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati.
Alisema hoja ya Tanzania ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa kwa vile tatizo kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwepo kati ya Cameroon na Nigeria.

CHANZO: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment