KAMBI YAKE YAPETA UWT, SASA WAJIPANGA UVCCM, WAZAZI
KAMBI
ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa imeendelea kuyanyanyasa
makundi mengine ndani ya CCM, ambayo yamekuwa yakijipanga kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu wa 2015.Kambi ya kiongozi huyo ni kama imehamia Dodoma ili
kuhakikisha watu wake wanashinda katika chaguzi za viongozi wa juu wa
jumuiya za CCM baada ya kufanikisha kile inachodai kuwa ushindi mkubwa
katika ngazi za wilaya na mkoa kutokana na watu wake wengi kushinda.
Wapambe
wa Lowassa wakiongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na
Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), Hussein Bashe wapo
Dodoma kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya
Wanawake (UWT) na wataendelea kuwapo mpaka jumuiya zote zitakapokuwa
zimefanya uchaguzi huo.
“Hapa kazi ni moja tu, hakuna kulala
maana tukilala tutajikuta tumewekwa pabaya. Tumefanikiwa UWT na sasa
tunaelekeza majeshi yetu UVCCM... lazima tuhakikishe tunakomesha uonevu
wa kuitana magamba mwaka huu,” alisema mmoja wa wapambe wa Lowassa juzi
usiku.
Matokeo ya uongozi wa juu wa UWT yameongeza matumaini kwa
kambi hiyo ambayo imezoa zaidi ya asilimia 80 ya viongozi katika jumuiya
hiyo yenye ushawishi mkubwa katika uamuzi mbalimbali wa chama hicho.
Mwenyekiti
wa UWT Taifa, Sophia Simba ambaye alitetea vizuri nafasi yake na Makamu
wake, Asha Bakari Makame wanatajwa kuwa katika kambi hiyo huku wajumbe
saba kati ya tisa waliochaguliwa kuiwakilisha jumuiya hiyo katika
Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho, wakiwa waumini wa kambo
hiyo.
Walioshinda nafasi za ujumbe wa NEC ambao wanatajwa kuwa
wafuasi wa Lowassa ni pamoja na Mbunge wa Ukonga, Eugen Mwaiposa, Waziri
wa zamani wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga na Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana.
Wengine ni wabunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo, Zainabu Kawawa, Mary Mwanjelwa na Subira Mgalu.
Wajumbe
wawili ambao ni pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene yeye
anatajwa kuwa hana kundi lolote wakati Mbunge wa Viti Maalumu, Betty
Machangu ambaye anatajwa kwamba alikuwa akimuunga mkono Mbunge wa Same
Mashariki, Anna Kilango Malecela.
Kilango ambaye alikuwa akiungwa
mkono na makundi ya watu waliojipambanua kuwa wapambanaji na ufisadi,
aliangushwa vibaya na Simba kwa zaidi ya kura 400 katika kinyang’anyiro
cha nafasi ya Mwenyekiti wa UWT.
Vigogo wengine wanaotajwa kuwa na
kambi katika kinyang’anyiro hicho cha urais wa 2015 ni Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambao katika uchaguzi wa
jumuiya za CCM nguvu zao zinaonekana kuwa si kubwa kama ilivyotarajiwa.
JK awapasha viongozi UWT
Mwenyekiti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete juzi usiku aliwatolea uvivu viongozi wa
UWT, akiwataka kuchukua hatua za kumaliza nyufa zilizosababishwa na
uchaguzi uliomalizika Jumamosi iliyopita.
Rais Kikwete alisema
viongozi waliochaguliwa wakiongozwa na Simba ambaye pia Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wachukue hatua kuondoa makundi
ambayo yanatokana na uchaguzi.
“Hii jumuiya siyo yenu, ni ya
wanachama kwa hiyo baada ya uchaguzi lazima muwe tayari kufanya kazi na
kila mmoja, isije ikawa ni wale marafiki zako tu maana ikiwa hivyo
utamteua hata kama uwezo hana,” alisema Kikwete alipokuwa akifunga
mkutano huo wa uchaguzi mjini Dodoma.
Alikemea tabia ya chuki
inayojengwa na uchaguzi akisema inatokana na viongozi walioko katika
nafasi mbalimbali za uongozi kudhani kwamba wanazimiliki binafsi.
“Hupaswi
kumchukia mtu eti kwa sababu amegombea nafasi fulani, hakuna nafasi ya
mtu, nafasi zote ni za chama, kwa hiyo kama ulikuwa mwenyekiti, uongozi
wako unakoma pale tunapotangaza upya uchaguzi,” alisema Rais Kikwete na
kuongeza:
“Tukishatangaza kila mwanachama mwenye sifa anakuwa na
haki ya kugombea nafasi hizo, sasa wewe usimchukie na kumuuliza eti kwa
nini unagombea nafasi yangu, siyo nafasi yako, hii ni nafasi ya chama.”
Alikemea
tabia ya baadhi ya viongozi au wagombea kuwajengea chuki wale ambao
hawakuwaunga mkono, na kwamba anayefanya hivyo hapaswi kuwa kiongozi.
Alisema
kiongozi wa aina hiyo daima ataongoza kwa makundi, akiwapenda wale
waliomuunga mkono na kuwatenga wale ambao walikuwa na mtazamo tofauti
jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa jumuiya na chama kwa jumla.
“Kila
mwanachama ana uhuru wa kumuunga mkono mtu anayempenda, sasa wewe
unapomkasirikia na kumjengea chuki unamaanisha nini? Demokrasia maana
yake ni kila mmoja wetu kumchagua mtu anayeona anafaa,” alisema.
Alitoa
mfano kwamba baada ya yeye kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM
mwaka 2005 na baada ya uchaguzi uliompa ushindi, aliwateua wale
waliokuwa washindani wake katika Baraza la Mawaziri, akiwamo Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya.
“Mwandosya
tuko naye hadi leo, hata wale waliokuwa wakinipinga na wengine
walinifanyia mambo ya ajabu kwelikweli, lakini hayo yote inafika mahali
unaweka kando maana huwezi kuongoza nchi kwa kuwateua marafiki zako tu,”
alisema Kikwete.
Uchaguzi UVCCM leo
Rais Kikwete leo
anatarajia kufungua Mkutano wa Nane wa UVCCM utakaofanyika katika Chuo
cha Mipango, Dodoma huku vita kubwa ikitarajiwa katika uchaguzi kwa
misingi ya kambi za urais kuelekea 2015.
Vita kubwa katika uchaguzi
huo ni katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambayo inawaniwa na Paul
Makonda, Mboni Mhina na Ally Salum Hapi, wakati nafasi ya Mwenyekiti
inawaniwa na Sadifa Juma Khamis, Rashid Simai Msaraka na Lulu Msham
Abdallah.
Katika nafasi ya umakamu, Makonda anaungwa mkono na
kambi ya Membe, wakati kambi ya Lowassa imeamua kuelekeza nguvu zake kwa
mwanadada, Mboni. Kambi hiyo pia inamuunga mkono Sadifa anayegombea
nafasi ya Uenyekiti.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema
jumuiya yake inafuatilia mienendo ya wagombea wote na wapambe wao na
kwamba watakaobainika kukiuka taratibu za uchaguzi watachukuliwa hatua.
Akizungumzia
suala la rushwa ambalo linaonekana kuiandama CCM pamoja na jumuiya
zake, Shigela alisema: “Katika hilo tumejipanga vizuri kukabiliana
nalo.”
“Mfano mzuri ni kule Zanzibar, katika Mkoa wa Mjini
Magharibi tumetengua nafasi za wajumbe wawili wa Baraza, hii ni
kuonyesha kuwa hatutanii lazima watu wawe waadilifu,” alisema.
Kwa
mujibu wa Kanuni ya Umoja wa Vijana, mkutano huo utakuwa chini ya
Uenyekiti wa Benno Malisa kwani kanuni inasema kama mwenyekiti si
mgombea, basi ndiye atakayeongoza mkutano huo.
Mkutano huo pamoja na kuchagua viongozi wa UVCCM, pia utapitisha katiba mpya ya jumuiya hiyo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment