Monday, October 15, 2012

Mdahalo wa jinsia waibua changamoto nyingi

Elimu kwa watoto wa kike bado ni tatizo kubwa katika Mkoa wa Pwani kutokana na wazazi kuthamini mdoa za utotoni.

Suala hilo ni moja ya changamoto zilizojitokeza katika mahadalo kuhusu jinsia ulioandaliwa na Asasi za Kiraia za Wilaya ya Bagamoyo (BANGONET) na kufanyika katika kijiji cha Yombo, Kata ya Yombo wilayani humo juzi.

 Akiwasilisha mada kuhusu changamoto za kijinsia, mwezeshaji katika mdahalo huo, Abraham Salim, alisema kuwa fursa ya elimu kwa mtoto wa kike mkoani Pwani ni tatizo kubwa.

“Katika fursa za elimu sera inatoa usawa wa mtoto wa kiume na kike kupata elimu, lakini Pwani wa kike wanaishia elimu ya msingi,” alisema Salim na kuongeza:

“Ndoa za utotoni ni kikwazo, wengi wanazuiliwa na wazazi kufanya vizuri katika mitihani. Wazazi wanashiriki kwa namna moja au nyingine.”

Alisema kuwa wazazi wanafanya kila njia watoto wao wafanye vibaya mitihani ili waolewe na kwamba mahari inakuwa imeshatolewa wakati mtoto anasona na baadhi ya watoto wa kike wanakuwa wanafahamu na wengine bila kufahamu.

Alitolea mfano kwa mtoto mmoja wilayani Kisarawe ambaye alifaulu mtihani wa darasa la saba, lakini mzazi wake alikataa ajiunge na masomo ya sekondari akidai kuwa hajui kusoma na kuandika.

Alisema kuwa baada ya kufuatiliwa ili binti yake aendelee na masomo, mzazi huyo aliamua kumhamisha eneo hilo.

Salim pia alisema kuwa changamoto nyingine inayokwamisha usawa wa jinsia mkoani Pwani ni nila na desturi. Alisema kuwa katika suala la uzalishaji, mwanaume anachukuliwa kuwa ndiye mtafutaji na mwanamke anaishi kama mpokeaji.

“Pwani inahalalisha kuwa mke hawezi kufanya kazi ila ataishi kwa nguvu za mumewe,” alisema Salim.

Aidha, alisema kuwa hakuna usawa wa jinsia katika umiliki wa mali za familia na kusema kuwa baadhi ya wanaume wa Mkoa wa Pwani wana tabia ya kutoweka nyumbani baada ya kuuza mazao na wanaporejea wanakuja na mke mwingine.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Yombo, Salim Juma Mavaga, alisema kuwa wananchi wa kata yake wamefurahi kupata mdahalo huo ambao uliwajumuisha watu wengi kuzungumzia mambo ya kijinsia na kupendekezo kuwa midahalo hiyo iwe endelevu.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Yombo, Xavery Mtumze, alisema kuwa zipo changamoto nyingi katika kijiji chake dhidi ya usawa wa kijinsia, likiwamo suala la urithi wa mali. Alisema urithi wa mali kama mashamba unawanifaisha watoto wa kiume tu.

Akiufungua mdahalo huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya yan Bagamoyo, Ahmed Kipozi, Mratibu wa Elimu wa kata hiyo, Tatu Libwangu, aliipongeza BANGONET na kuongeza kuwa anaanini kuwa itaendelea kuhamasisha jamii kwa njia ya midahalo na nafasi ya kijinsia ili jamii yote ya Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla ielimike na kuheshimu usawa na h
aki za kijinsia.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment