Thursday, April 26, 2012

Baregu: Ni Muungano wa kipekee, ni muhimu kuuimarisha

Mwandishi wa Makala haya, HAWRA SHAMTE alizungumza na Profesa wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Mwesiga Baregu kabla hajateuliwa kuwa mjumbe wa Tume ya Katiba. 
Kwa mawazo yake yeye Muungano unapaswa kujadiliwa kwa uwazi mpana kabisa na kwamba wakati huu ambao Watanzania wameingia katika mchakato wa kutafuta katiba mpya ni wakati mwafaka wa kuujadili muungano na kuamua tunataka uwe wa aina gani.

Swali:  Profesa Mwesiga Baregu, nini mawazo yako kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?
Baregu:    Ikumbukwe kwamba sisi ambao ni wazee kidogo tumekuwa kwa umri mkubwa tukiwa Watanzania. Utanganyika wa uhuru tumeishi nao kwa miaka mitatu, utanganyika sisi tunaoujua huko nyuma ni utanganyika wa ukoloni, Tanganyika ile ya kina Edward Twining na magavana wengineo.
Leo hivi mimi nikiwasikia vijana wakisema kuwa “tunaitaka Tanganyika irudi” mimi najiuliza, hivi wanataka Tanganyika gani? Ya magavana Edward Twining au ni hii ambayo tulikuwa nayo kwa miaka miwili mitatu, au ni ipi Tanganyika wnayoitaka ambayo wala hawakuiishi, ile ya mkoloni hawaijui, ile ya miaka miwili mitatu hawaijui, sasa wanataka Tanganyika gani?
Mimi kwa miaka yangu na umri wangu huu najua mimi ni Mtanzania.  Mimi nisingependa kuja kupita wakati ambao ninaishi kama Mtanganyika, maana yake ni Utanganyika gani huo?  Siujui.  Na nakueleza wazi wazi kwamba mimi nitakuwa na matatizo kisaikolojia kujitambua kama Mtanganyika, nitapata shida sana.
Mwaka 1968 wakati wa maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa Azimio la Arusha nilikuwa mwanafunzi Uingereza, nilikja hapa, nikaenda kumuona Mwalimu Nyerere halafu tukapelekwa kumuona marehemu Abeid Karume.  Nadhani Karume alikuwa mwana-Muungano mkubwa kuliko Mwalimu Nyerere.
Tulimuuliza Mwalimu Nyerere nini maana ya Serikali mbili?  Akatujibu nendeni mkamuulize karume.
Tukaenda kumuuliza Karume, akasema; “serikali mbili ni kitu alikileta Mwalimu, mimi nilikuwa nasema tuwe na serikali moja nay eye Mwalimu ndiye awe Rais na mimi ningekuwa msaidizi wake, akakataa.  Akawaleta wanasheria wake wakavurugavuruga.  Mpaka sasa mimi serikali mbili sijazielewa vizuri.”
Hivyo huo ndio uliokuwa msimamo wa Karume, tuwe na serikali moja.
Mimi nataka kusema kwamba Wazanzibari na watu wa Bara, wa kizazi change na vizazi vya baadaye tunaujua Utanzania.  Sasa katika mchakato huu wa Katiba Mpya tuamue kama tunataka kuendelea kukaa pamoja kama kitu kimoja?  Nadhani hilo ni la msingi, halafu tujadili tukae vipi na iweje.
Mimi nadhani huu ndio wakati mwafaka wa kuzungumza yote yanayohusu Muungano.  Kwa mara ya kwanza Watanzania wajipe nafasi ya kuzungumza na kujenga muungano wa maridhiano.
Kwanza tukubaliane kama tunataka muungano na kutambua kwanini tunautaka, lakini pili; uwe wa namna gani, serikali mbili au tatu, lakini kwanza tujenge hoja.  Ukiniuliza mimi nitajenga hoja ya kuwapo kwa serikali moja.  Mimi ni Pan Africanist nataka muungano wa Afrika nzima.
Mwalimu Nyerere miaka miwili kabla hajafariki alipokwenda Accra Ghana wakati wa maadhimisho ya miaka 40 ya Uhuru wa Ghana, akasema kwamba yeye alimpinga Kwame Nkurmah kwa suala la serikali moja, lakini akawataka radhi Waghana kwamba yeye alikuwa amekosea na Nkrumah alikuwa sawa. Kwamba hii njia tuliyokwenda ya Umoja wa Afrika haijatupeleka popote na haitatupeleka popote.   Akasema Afrika bila kuungana haitakuwapo ( Without Unity, there is no future for Africa).  
Katika mjadala wetu huu wa katiba, matumaini yangu ni kwamba hilo tutaliweka maanani, angalau tuelewe umuhimu wa muungano wa Tanzania.  Sasa hivi sisi tulionao ndani tunauchukulia kama upuuzi, lakini umekuwa ni mfano mkubwa siyo tu kwa Afrika lakini kwa ulimwengu mzima.

Swali:  Muungano wetu tunasema kuwa ni wa kipekee, laini  muundo wake haueleweki, kwa sababu huu muungano wetu ukiuweka kwenye ‘Unitary’ hauko na ukiuweka kwenye ‘Federal’ haupo, je, huu ni muungano wa namna gani?
Baregu:   Kila muungano ni wa kipekee, kwa sababu kila muungano una historia yake.  Hakuna Ujerumani mbili, Ujerumani ni muungano lakini haufanani na Marekani.  Mpaka sasa baada ya miaka 100 na kitu bado wana mivutano ndani ya Ujerumani yao.
Ukienda Marekani; walipigana vita Kaskazini na Kusini, watu wa Kusini wakashindwa, ndiyo wakatunga katiba wakawa na Muungano,  Kila muungano una historia yake, una mazingira yaliyouzaa na una matatizo yake.
Mengine imesambaratika, mwanzoni kulikuwa na  Guinea, Ghana, Mali Federation hakuna tena, yalikuwa majaribio na yakashindwa.
Sasa mimi nasema kwamba Muungano ni moja ya changamoto tulizonazo.  Kuhusu hilo suala la Muungano kuwa haueleweki,  ni sisi tu kwa maamuzi yetu ndio tutakaounda muungano unaoeleweka kwetu na siyo lazima ueleweke kwa mataifa mengine, utaeleweka kwa kuangalia maslahi ya Watanzania, kama sisi tukiuelewa ‘what do we care kama ulimwengu hauuelewi?
Waingereza wakiangalia Ujerumani hawaielewi; lakini Ujerumani nayo ikiangalia uhusiano kati ya Ireland, Wales, Scotland vilevile hawaielewi Uingereza.  Kwa hivyo sisi tunapaswa kuongozwa na matakwa na maslahi ya Watanzania na wale ambao tuna upeo mkubwa zaidi tuangalie maslahi ya Afrika kwa ujumla, halafu ndiyo tuunde mfumo na utaratibu ambao utatufaa.
Chochote tutakachokiunda, kitategemea ni kiasi gani tumekuwa na  maelewano, maridhiano kwamba hiki ndicho chombo kitakachotufaa, mimi matumaini yangu ni kwamba tutazungumza kwa uwazi lakini tukiwa tunaelewana kwamba tuna historia ya pamoja kiasi cha kwamba ukatokea msemo usemao kuwa ‘ngoma ikipigwa Zanzibar, inachezwa Maziwa Makuu.’

Swali:  Profesa wewe unapendekeza kwamba tuwe na umoja ikiwezekana hata wa Afrika, lakini umoja wa kikanda tu umekuwa na matatizo, hata tukizungumzia Shirikisho la Afrika Mashariki, tumekuwa tukipata shida kuukamilisha.  Je, huoni kama tunazungumzia umoja wa kiyutopia tu, wa kimawazo?
Baregu: Hakuna kitu kizuri kitakachoanza bila mawazo, kwanza lazima kijengwe katika mawazo, ndiyo maana nasema itategemea mawazo ambayo tutabadilishana kwa umakini bila jazba, tukaelewana siyo tu kwa maslahi ya leo, siyo tu kwa maslahi ya Zanzibar peke yake.  Lakini kwanza lazima tukubaliane, je, tunataka muungano?  Kama tunautaka hatuwezi kushindwa kuunda muungano tutakaoutaka.
Kuna minong’ono inajitokeza tokea eti Zanzibar inataka uhuru, ili iweze kuungana na Oman na kadhalika.  Hii minong’ono iletwe kwenye meza tuizungumze. Tuzungumze kama watu waliokomaa, kama watu wenye uwezo wa kujenga hoja, kama watu wenye uwezo wa kubadilishana mawazo, kama watu wenye uwezo wa kuona maslahi yetu ya muda mfupi na muda mrefu na tukajenga vyombo na taratibu za kukuza na kujenga maslahi yetu ya pamoja, ya kujenga na kukuza maslahi ya Zanzibar pekee na hata yale ya Tanzania Bara.
Hivi karibuni tulikuwa tunazungumza suala la maeneo ya muungano na mambo yasiyokuwapo katika muungano, yote haya tuna nafasi ya kuyazungumza na hata tukatengeneza mambo ya muungano mapya kabisa. Haya yote tunaweza kuyazungumza katika Tume ya Katiba.

No comments:

Post a Comment