Imeandikwa na: Peter Saramba, Arusha
HALI ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa
(UVCCM), Mkoa wa Arusha imeanza kugubikwa na sintofahamu baada ya jana
watu wasiojulikana kuvamia na kuzifunga kwa kufuli ofisi zake za mkoa
kuzuia viongozi kuingia.
Pamoja na kufunga ofisi hizo, watu hao
wanaodaiwa kuvamia eneo hilo kati ya Saa 4:30 na 5:00 usiku wa kuamkia
jana pia walibandika mabango ya kumkataa Katibu wa UVCCM Mkoa wa
Arusha, Abdallah Mpokwa wakimtuhumu kutozingatia maslahi ya jumuiya
katika uongozi wake.
Miongoni mwa mabango yaliyobandikwa kwenye
mlango na madirisha ya ofisi hizo zilizoko eneo la Kaloleni jijini
Arusha yalisomeka “Umoja wa vijana wa CCM Mkoa wa Arusha, hatumtaki
Abdallah Mpokwa kwa kuwa mnatumika na Lowasa na si kwa Kanuni za UVCCM”
Bango
lingine lililobandikwa mlangoni lilisisitiza tuhuma na madai ya
kuondoka na Sh2 milioni zilizochangwa na waliokuwa wabunge wa Jimbo la
Arusha mjini, Felix Mrema na mwenzake wa Arumeru Magharibi, Elisa Mollel
zinazoelekezwa dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, James Ole
Millya aliyehamia Chadema.
“Abdallah Mpokwa na James Millya rudisheni pesa zetu za Saccos ya vijana wa CCM Arusha” ilisomeka moja ya bango.
Waliobandika
mabango hayo zaidi ya manne walimtaka katibu huyo wa UVCCM kuhamia
Chadema kumfuata Ole Millya badala ya kuendelea kubaki ndani ya CCM huku
akimtetea mtu aliyehamia chama hicho kikuu cha upinzani.
Hadi jana hakuna kundi lolote kati ya makundi mawili ya vijana yanayosigana lililodai kuhusika na ufungaji wa makufuli hayo.
Lakini
baadhi ya vijana walioonekana dhahiri kumpinga Ole Millya walijitokeza
kuzungumza na waandishi wa habari kulaani kauli ya Mpokwa waliyodai
ililenga kumsafisha aliyekuwa mwenyekiti wao.
Akizungumza na
waandishi wa habari nje ya ofisi za CCM mkoa zilizo hatua chache kutoka
zile za UVCCM, Ally Shabani maarufu kwa jina la ‘Majeshi’
aliyejitambulisha kuwa ni katibu wa Jumuiya hiyo, Kata ya Moivo,
wilayani Arumeru alidai kuna ushahidi unaothibitisha fedha hizo kutolewa
na kukabidhiwa chini ya uongozi wa Ole Millya mwaka 2008, lakini hadi
leo hakuna taarifa zozote za kuanzishwa kwa Saccos hiyo.
“Kauli
ya Mpokwa kuwa UVCCM haijawahi kuwa na mradi wa Saccos wala kuwapo
kumbukumbu za Sh2 milioni zilizotolewa na waheshimiwa Felix na Elisa ni
upotoshaji mkubwa kwa sababu fedha hizo zilitolewa hadharani kwenye
mkutano wa Baraza lililofanyika Karatu,” alisema Shabani.
Kada
huyo wa CCM ambaye ni miongoni mwa viongozi wa UVCCM waliopewa onyo kwa
kwenda kinyume na taratibu za chama hicho mwishoni mwa mwaka jana
alihoji kwanini katibu huyo anajitokeza kumtetea Ole Millya ambaye ndiye
alipaswa kujibu tuhuma dhidi yake.
“Uamuzi wa vijana kufunga
ofisi hiyo yao kama tunavyoshuhudia hapa ni sahihi kwa sababu tamko la
kumtetea Ole Millya lililotolewa na katibu halina mashiko na kamwe sisi
vijana wa Arusha hatuko tayari kuendelea kuongozwa na katibu
anayetumikia watu binafsi badala ya chama, aende huko Chadema kwani ni
mamluki” aliongeza Shabani huku akikana kuhusika na ufungaji ofisi.
Kijana
mwingine Masoud Rajabu ambaye kama Shabani alimrushia madongo Mpokwa
huku pia akikana kuhusika na zoezi la kufunga ofisi na kubandika mabango
alimwomba mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Steven Wassira kufika haraka
mkoani hapa kuokoa jahazi kama alivyofanya mwaka jana wakati kulipotokea
minyukano kati ya makundi hayo mawili.
Hata hivyo Rajabu
alimwonya Mlezi huyo kuacha tabia ya kufika na kukutana na viongozi
pekee aliodai humpotosha na badala yake safari hii akubali kukutana na
vijana kwenye kikao cha wazi ili wamweleze jinsi viongozi wengi wa chama
hicho mkoani Arusha wanavyoshiriki kukiangamiza na kukipa umaarufu
Chadema.
Wakati vijana hao wakikana kuhusika na waliofunga ofisi
hizo, muda wote walionekana kuwapanga wenzao kuzilinda kuhakikisha
hakuna mtu anayezifungua hali iliyotishia uwezekano wa kutokea machafuko
iwapo kundi linalomuunga mkono Mpokwa lingejitokeza kuvunja makufuli na
kuondoa mabango.
Hivi karibuni, akizungumza na waandishi
wahabari ofisini kwake juzi, Mpokwa akiwa na baadhi ya wajumbe wa Baraza
la vijana Mkoa wa Arusha alikanusha aliyekuwa mwenyekiti wake, Ole
Millya kuhamia Chadema na Sh 2milioni za mradi wa Saccos la vijana.
Pamoja
na kukana tuhuma hizo zilizotolewa na mjumbe wa Baraza la UVCCM Taifa,
Mrisho Gambo na Kenenedy Mpumilwa ambaye ni mjumbe wa baraza la mkoa,
Mpokwa pia alisema Ole Millya hakupaswa kukabidhi ofisi kwani hakuwa
mtendaji wa kila siku bali mwongoza vikao, kauli ambazo zimewakera
vijana hadi kumfungia ofisi na kumtaka aondoke
No comments:
Post a Comment