Friday, April 27, 2012

Uzazi wa mpango suluhu vifo vya uzazi


MAWAZIRI wa Afya wa nchi za Afrika walipokutana Mei 2009, mjini Addis Ababa, Ethiopia waliridhia suala la kuzindua rasmi kampeni ya kuharakisha kupunguza vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi na afya ya watoto katika nchi zao.

Kampeni hiyo, Campaign for Accelerated Reduction of Maternal Mortality In Africa (CARMMA), ina malengo ya kuongeza kasi katika kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na vya watoto wachanga, ili kufikia malengo ya milenia namba 4, na 5, ifikapo mwaka 2015.

Kaulimbiu ya kampeni hiyo, ‘No woman should die while giving life Africa Cares’ ikiwa na maana ya Afrika inajali: “Asife mwanamke wakati analeta kiumbe hai”.

Baada ya uzinduzi huo, kila nchi mwanachama ilitakiwa izindue kampeni yake katika nchi zao kwa lengo la kukabiliana na vifo vinavyotokana na uzazi pamoja na watoto wachanga baada ya kuzaliwa.

Madhumuni ya kampeni  hiyo ni kuhamasisha jamii  ichangie katika juhudi za kitaifa za  kuharakisha kupunguzwa kwa vifo  vya wajawazito na watoto na Tanzania ilizindua kampeni hiyo Juni 6, mwaka jana.

Katika uzinduzi uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam ambao ulifanywa na Waziri wa Afya na Usitawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, kaulimbiu yake ilikuwa, “Tanzania inajali - mwanamke asife kwa ajili ya kuleta kiumbe hai; na mtoto asife kwa sababu zinazozuilika”.

Kikwete alisema shughuli ya uzinduzi huo ilikuja wakati mwafaka, kwani serikali ipo katika mchakato na inayo mkakati mahususi wa afua, inayotekelezeka.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Dk. Alberic Kacou, alisema kutotumika kikamilifu kwa vidonge vya uzazi wa mpango ni sababu kubwa ya vifo vinavyotokana na uzazi Tanzania.

Dk. Kacou akaishauri Serikali kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango ili kudhibiti mimba zisizohitajika kwani tafiti zinaonyesha wanawake wengi wanapenda kutumia mpango huo lakini hukosa huduma hizo.

“Wanawake wengi wa Tanzania wanapenda kutumia dawa za uzazi wa mpango kwa ajili ya kutoa nafasi kati ya watoto na wengine kudhibiti ukubwa wa familia, lakini kwa bahati mbaya hawapati huduma hizo,” anasema Dk. Kacou na kuongeza:

“Tumeweka lengo la kufikisha asilimia 60 kwa wanaotumia uzazi wa mpango ifikapo mwaka 2015, lakini kwenye ripoti ya Tafiti ya Demografia na Afya inaonyesha hatujafika hata nusu ya makadirio hayo ya mwaka 2015”.

Utafiti wa Hali ya Maisha na Afya  wa mwaka 2004/05 ulionyesha ni asilimia 47 ya wajawazito walijifungulia katika vituo vya afya na utafiti kama huo mwaka 2010, umeonyesha ongezeko la kufikia hadi asilimia 50.

Pamoja na mikakati hiyo, Tanzania imeanza kuona mafanikio katika kupunguza vifo vitokanavyo na matatizo ya wazazi kutoka wanawake 578 kwa kila vizazi hai 100,000, kama ilivyokuwa mwaka 2004, hadi kuwa 454 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2011.

Mafanikio hayo ni sawa na punguo la vifo 8,100 hadi 6,800 kila mwaka. Ili kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia, inabidi vipungue hadi view 193 kwa kila mizao hai 100,000.

Vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 vimepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka kumi iliyopita, kutoka vifo 147 kwa kila vizazi hai 1,000 kama ilivyokuwa mwaka 1999 hadi 81 kwa kila vizazi hai 1000 mwaka ilipofikia mwaka 2010.

Punguzo hilo ni la asilimia 45, ikilinganisha na ilivyokuwa mwaka 1999. Ili kufikia lengo la milenia, vifo vya watoto wa umri wa chini ya miaka 5 vinatakiwa kupungua hadi 54 kwa kila vizazi hai 1000.

Idadi ya vifo vya watoto wa umri huo vimepungua kutoka 223,000 hadi 145,000 kwa mwaka na vya watoto wa umri wa chini ya mwaka mmoja vimepungua kwa asilimia 49 kutoka 99 kwa kila 1,000 kama ilivyokuwa 1999 hadi 51 kwa kila vizazi hai 1,000 kufikia 2011.

Vifo vya watoto wachanga wenye umri wa chini vya mwezi mmoja vimepungua kwa kiasi kidogo kwa zaidi ya nusu ya walio chini ya mwaka mmoja, vikiwa ni 26 kwa kila vizazi hai 1,000. Vingi vinatokana na matatizo, vikiwa ya uzazi.

Mwaka 2008, Rais Kikwete alizindua Mpango kabambe wa kuongeza juhudi za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto (Road Map 2009-2015), ili kuhakikisha tunakuwapo muongozo wa utekelezaji.

Hivyo, Serikali imechukua hatua za kuongeza  idadi  ya wataalamu wa huduma za afya,  kwa kuongeza idadi ya vijana wanaodahiliwa kuingia vyuo vya afya na kufungua vyuo vipya.

Katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, wanafunzi waliodahiliwa kuingia katika vyuo hivyo iliongezeka mara nne, kutoka 1,013, mwaka hadi 2007, kufikia 6,713 mwaka 2010, lengo likiwa kufikia udahili wa wanafunzi 10,000 kwa mwaka, ifikiapo 2015.


Makala haya yameandaliwa na muungano wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayotetea kuboreshwa kwa huduma za uzazi wa mpango.

No comments:

Post a Comment