Aidan Mhando WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli, amezitaka wizara za Maji, Fedha, Nishati na Madini kuhakikisha hazikwamishi miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja Dar es Salaam kwa kuondoa vizuizi vyote vilivyopo ndani ya hifadhi, huku akitoa siku saba kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuondoa nguzo za umeme zilizopo kwenye hifadhi ya barabara. Dk Magufuli alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana, alipokuwa akitembelea miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara ambayo pia inahusisha mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam (Dart). Alisema ili kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa katika hali nzuri ya miundombinu, Serikali imetenga Sh288 bilioni zitakazotumika katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu. “Kuna miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara na madaraja Dar es Salaam, Sh288 bilioni zitatumika katika ujenzi wa madaraja na barabara za mabasi yaendayo kasi,” alisema Dk Magufuli na kuongeza: “Moja ya miradi mikubwa ambayo imeanza kufanyiwa kazi, ni ujenzi wa barabara ya Mwenge -Tegeta ambayo itagharimu Sh88 bilioni, ujenzi wa vituo vikubwa vya mabasi ambavyo vitagharimu Sh48 bilioni jambo ambalo litafanya kupunguza msongamano wa magari Dar es Salaam pindi ujenzi huo utakapokamilika.” Pia, Waziri Magufuli alibainisha kwamba ndani ya miradi hiyo kutakuwa na ujenzi wa barabara ya Kimara - Magomeni, ambayo itakuwa na njia sita barabara ya Magomeni -Faya itakuwa na njia nane, barabara ya Faya -Kivukoni itakuwa na njia nne na barabara ya Morocco itakuwa na njia sita. Dk Magufuli alisema ujenzi wa barabara hizo tayari mkandarasi amepatikana ambaye ni Kampuni ya Strabag ya nchini Ujerumani. Alisema mkandarasi huyo tayari amelipwa asilimia 20 ya fedha na kwamba, tayari hatua za mwanzo za ujenzi wa barabara hizo umeanza kufanyika. “Tunataka ujenzi wa barabara hizi uwe wa kasi na bora, ili kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kama tulivyopanga tayari mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Strabag Serikali imeshamlipa asilimia 20 ya fedha anazotakiwa kupewa,” alisema. Alisema ujenzi huo utajumuisha ujenzi wa barabara Mwenge -Tegeta ambayo tayari imeshakamilika na kilichosalia ni kukamilisha ujenzi wa madaraja 38, vituo 28 vya mabasi na madaraja matatu makubwa na kwamba, kufikia Mei mwakani utakuwa umekamilika. Katika hatua nyingine, Waziri Magufuli aliitaka Kampuni ya Strabag kuhakikisha inatoa ajira kwa vijana wa Dar es Salaam. Alisema hatavumilia kuona wakazi wa Dar es Salaam wanakosa ajira kwa sababu ya ubaguzi wa watu fulani, kwani kila sehemu ambayo kunakuwa na miradi mikubwa ni vyema wakazi husika wakapewa ajira. Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwamtumu Mahiza, aliwataka wakazi wa Dar es Salaam waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara kuondoka wenyewe kabla ya bomoabomoa haijawakuta. |
Thursday, May 3, 2012
Dk Magufuli atoa siku saba kwa Tanesco
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment