Thursday, May 3, 2012

Wanawake Newala wana shida kubwa kupata mali

Mary Sanyiwa, Newala

WANAWAKE Wilaya ya Newala mkoani Mtwara wamewalalamika wanaume wao wilayani humo kutokana na kutowashirikisha katika kutoa uamuzi badala yake hushirikishwa kwenye kilimo pekee.

 Mwenyekiti wa Asasi  inayotetea hakli za wanawake, Sophia  Mnyelenje alisema hayo alipoelezea shida mbalimbali zinazowakabili wanawake wa wilaya hiyo.Mnyelenje alisema wanawake  wilayani huo hawashirikishwi ipasavyo  katika kipindi cha mavuno na kwamba wengi kipindi hicho wanatelekezwa na waume wao.

Alisema baada ya kuanzishwa kwa asasi hiyo wanapokea kesi nyingi za kuvunjika kwa ndoa ambapo wao  wanawasaidia kwa kuwapa ushauri ili wanawake waweze kupata mali ambazo wamechuma na wanaume wao.
"Baada ya wanawake kuona asasi yangu walifurahi sana kupata mtetezi wao kwani wamehangaika kwa kipindi kirefu. Walikuwa wakihaha kupata ushauri wa kufahamu mambo mbalimbali ya kisheria", alisema Mnyelenje.

Aidha alieleza sababu inayochangia wanawake wengi kutopa haki zao za msingi kwamba ni kutokana na uelewa mdogo  wa  kujua rasilimali zao pamoja na ufuatiliaji.

Mwenyekiti huyo alisema wanaothirika zaidi ni watoto kwani hawapati malezi bora ya wazazi wao sambamba na kukosa elimu ambayo ingewasaidia katika maisha yao ya baadaye.

 Mwenyekiti wa asasi aliishauri Serikali kushirikiana kwa karibu na asasi zinazotoa elimu katika jamii ili kupunguza talaka za mara kwa mara wilayani humo.

No comments:

Post a Comment