JUMA lililopita, Mwandishi Wetu Fredy Azzah, alieleza jinsi jamii ya
wafugaji kutoka wilayani Simanjiro mkoni Manyara ilivyobuni mbinu mpya
ya kukeketa watoto wachanga.
Katika sehemu ya mwisho ya makala
hiyo, ambayo pamoja na mambo mengine Serikali inaeleza mikakati yake ya
kupambana na ukatili huo.
Diwani wa Kata ya Langai, Jackson
Lesikari anasema kuwa, kwa kiasi kikubwa vitendo hivyo ktika eneo lake
havipo, na kuwa wananchi wamebadilika baada ya kupatiwa elimu juu ya
madhara ya vitendo hivyo.
“Ukeketaji wameacha kabisa baada ya
kipewa elimu, watu wanaotoa elimu wanashirikiana na malaigwanani
(viongozi wa kimila wa Kimasai),” anasema Lesikari
Anasema kuwa
shirika lisilokuwa la kiserikali la Nafgem, linalotoa elimu juu ya
ukeketaji, kwa kiasi kikubwa limefanikiwa kupunguza tatizo hilo kwa
wanajamii hao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lolumorijei, Jeremia
Lemandi anasema kuwa katika eneo lake vitendo vya ukeketaji vimepungua
huku akisema kuwa, kwa kiasi kikubwa wanawake ndiyo wanaojua ukweli wa
vitendo hivyo kwani ndio huvitekeleza.
“Kinamama ndiyo wanakeketa, ukiwauliza ndiyo watakwambia vizuri,’ Lemandi.
Ingawa
Lemandi anasema hayo, watu mbalimbali wa eneo hili wanasema kuwa, mtoto
ni mali ya baba na wala mama hana sauti yoyote juu yake na hivyo baba
ndiye mwamuzi wa kila jambo kwa binti yake ikiwa ni pamoja na kuamua
akeketwe aole na mambo mengine kam hayo.
Naye Naomi Meshilieki
anasema kuwa, kwa kiasi kikubwa wanafunzi ambao wanaingia shuleni bila
kukekeketwa, hufanyiwa vitendo hivyo wakati wa likizo ama wakati
mwingine kusingia shuleni kuwa wanaumwa.
Mkuu wa Shule ya
Sekondari Simanjiro, Jacob Khahima anasema kuwa ni vigumu kuainisha
madhara ya ukeketaji kwenye elimu kwa kuwa vitendo hivyo hufanyika kwa
usiri mkubwa.
Lakini, Ofisa Elimu ya Msingi wa Wilaya hiyo,
Jackson Mbise anasema kwa kiasi kikubwa vitendo hivyo vinachangia katika
kudidimiza elimu katika eneo hilo.
Anasema kuwa, sababu
zinazochangia hali hiyo ni mafunzo ambayo mabinti hupewa wakati wa
kukeketwa ambayo huwafanya kujiona kuwa ni watu wazima na wanaweza
kufanya chochote.
“Wakitoka huku wanakuwa tayari wameondolewa
kwenye mazingira ya kishule shule, wanajiona sasa wao ni watu wazima
wapo tayari kutembea na wanaume na kujenga familia, elimu kwao huwa ni
kitu kidogo sana,” anasema.
Anasema kuwa, hali hiyo ndiyo sasa
husababisha mimba na wengine kuacha shule na kuolewa, mambo ambayo kwa
ujumla wake anasema yanaporomosha elimu katika eneo hilo.
Mrakibu
wa Polisi Wilaya ya Simanjiro (ASP), Felix Kikwala anasema kwa kiasi
kikubwa kuwakamata watu wanaotekeleza vitendo hivyo noi vigumu kwani
vinafanyika kwa usiri wa hali ya juu.
Ofisa Mradi wa shirika
linalotoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji, Nafgem, Michael Nyari,
anasema kwa kiasi kikubwa wanetoa elimu katika jamii ya eneo hilo juu ya
madhara ya vitendo hivyo.
Anasema moja ya changmoto
wanayokabiliana nayo nikuwa, jamii ya kimasai inaheshimu sana vitendo
vya ukeketaji hivyo wakati mwingine inauwa vigumu kuacha kabisa mila
hizo.
“Wamasai ni watu wenye siri sana, wanatekeleza hivi vitendo
sasa katika hali ya usiri na hata hao wanaofanyiwa kati ya mambo
wanayofundishwa ni kuwa wasiri na kutunza mila zao, wanaamini
wakizivunja wanaweza kulaaniwa hata wakapoteza maisha,” anasema Nyari.
Moja
ya mambo yanayoelezwa kuwa yanaweza kukomesha vitendo hivyo ni pamoja
na ngariba kupewa njia nyingine ya kuendesha maisha yao kwani wengi
wamefanya shughuli hiyo kwa kuwa hawakuwa na jingine la kufanya.
Jambo
linalothibitishwa na ngariba Kariayi anayesema kuwa, shughuli ya
ukeketaji ndiyo inayomwezesha kutunza watoto 10 alioachiwa na mume wake.
“Sasa
hivi kwanza mimi nimeshakuwa hata mkirsto, nikiweza kupata kitu kingine
cha kufanya nitaachana hata hii kazi,” anasema ngaiba huyo.
Hata
hivyo, pia wanasiasa wanatakiwa kubadilika na kuwa na ujasiri wa kukemea
vitendo hivyo badala ya kuwa na sura tofauti katika kutekeleza vita
dhidi ya vitendo hivyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
hiyo, Patrick Saduka anasema kuwa kwa sasa wanafanya uchunguzi ili
kujiridhisha kama kweli kuna vitendo vya ukeketaji kwa watoto.
“Tulikuwa
na kikao hivi karibuni tukishauriana jinsi ya kujiridhisha na taarifa
zilizopo, tulifikiri labda watoto wakija kiliniki wakaguliwe lakini
tukaona kuna changamoto zake, kwa hiyo bado tunaumiza kichwa kuangalia
jinsi ya kubaini hilo,” anasema Saduka.
Anasema pia kuwa katika
kupambana na suala hilo mmoja wa ofisa wa Halmashauri hiyo anashirikiana
kwa ukaribu na shirika lisilo la kiserikali la Nafgem ili kupata
maelezo ya kina juu ya ukubwa wa tatizo hilo.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Kijakazi Mtengwa anasema
kuwa Wizara inatambua kuwa katika maeneo mbalimbali ambapo jamii
ilikuwa ina utamaduni wa kukeketa wanawake, sasa wamehamia kwa watoto
wachanga.
Anaeleza kuwa, wanatambua suala hilo linafanyika lakini
sababu kubwa ikiwa ni kwa sababu watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo
hawawezi kusema juu ya unayama huo wanaofanyiwa.
“Hilo tunalijua baada ya watoto kupelekwa hospitali na manesi wanatambua kuwa tayari wamekeketwa,” anasema Mtengwa.
Anaongeza
kuwa, tofauti na njia hiyo huwezi kubaini vitendo hivyo kwa njia
nyingine kwa kuwa vitendo hivi hufanyika kwa uficho mkubwa.
“Mtoto
wa mtu kabwebwa tu, huwezi kujua kama amekeketwa ama vipi, kwa hiyo
taarifa nyingi tulizo nazo ni hizi kutoka hospitalini, kwa hiyo niseme
tu kuwa tuna uthibisho wa kuwa kwa sasa watu wanakeketa watoto
wachanga,” anaeleza Mtengwa.
Anasema kwa kuwa suala la ukeketaji
limekaa katika jamii kwa muda mtrefu, inakuwa ni vigumu kulimaliza kwa
mara moja hivyo njia pekee inayohitajika kwa sasa ni kuendelea kutoa
elimu juu ya madhara ya vitendo hivyo.
“Hata ukisema unampa
ngariba cherehani ili aachane na kazi yake ya kukeketa, unaweza kujuma
mpaka anafikisha umri alionao ameshawafundisha watu wangapi kukeketa,
mwisho wa siku anachukua cherehani anampa mwanaye na yeye anaendelea na
shughuli yake, kwa hiyo kikubwa cha kufanya ni kutoa elimu zaidi,”
anasema Mtengwa.
MWANANCHI NEWS PAPER
No comments:
Post a Comment