Na Burhani Yakub, Tanga
“NINAOMBA jamii inisaide nisome,
niokoeni na ukatili huu wa wazazi wangu wanaotaka kuniozesha tena kwa
nguvu kwa mwanaume asiye chaguo langu.
"Wazazi wangu wamesahau
kwamba mimi bado ni mwanafunzi, najisikia vibaya kweli nikose kusoma
kwa sababu tu ya ndoa, mimi siwezi kukubali kuolewa.”
Hiyo ni
kauli na malalamiko ya mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya
Msingi Kingo, Kata ya Masagaru Wilayani Kilindi, Ngaisi Islamoi (13)
ambaye anaishi kama mkimbizi kwa diwani wa Kata ya Masaguru, Mohammed
Makengwa kwa muda mrefu sasa.
Binti huyo anakizungumzia kwa huzuni kisa cha baba yake mzazi kujaribu kumwozesha kwa mwanaume kwa mahari ya ng’ombe watano.
Akiwa
mafichoni nyumbani kwa Diwani Abubakari Makengwa, mwanafunzi huyo
anaeleza historia yake kuwa alizaliwa mwaka 1999 mkoani Manyara akiwa
mtoto wa pili katika familia ya Islamoi Kuresoi na mama Helena
Lolamatu.
Anasema baadaye wazazi wake walihamia Kilindi kwa
ajili ya kutafuta ardhi ya mifugo pamoja na kilimo ndipo wakafikia
kitongoji cha Chang’ombe, Kijiji cha Kwamba Kata ya Masagaru.
Wakiwa
kijijini hapo wazazi wake walimwandikisha yeye na kaka yake Memarut
Islamoi katika Shule ya Msingi Kingo na mwaka juzi mdogo wake aitwaye
Loynyake pia aliandikishwa shuleni hapo.
“Miaka yote nilikuwa
nahudhuria masomo bila matatizo na nashukuru Mungu maendeleo yangu
darasani yalikuwa yakienda vizuri na walimu walinisifu kwa kujitahidi,”
anaeleza.
Anaongeza kuwa mwanzo wa mateso yake ulikuwa mwaka jana
wakati akiwa darasa la sita ambapo mwezi Oktoba baba yake alimwamuru
aache shule na kumjulisha kwamba anatakiwa kuolewa wakati wowote kwani
tayari ameshaanza kutolewa mahari ya ng’ombe.
“Baba aliniambia
wazi wazibila kificho kwamba lazima niache shule ili niolewe na kijana
wa kutoka familia ya mzee mmoja mfugaji wa asili ya Kimasai kama sisi
ambaye amepangiwa kulipa ng’ombe watano kama mahari na kwamba tayari
ng’ombe dume mmoja alishakuwa ametolewa,”anasema.
Binti huyo
mwanafunzi huyo anasema alipoelezwa kuhusu suala hilo la kuolewa
hakumjibu chochote baba yake kwa kuwa kwa mujibu wa mila na desturi za
kabila lao msichana au hata mwanamke haruhusiwi kujibishana na mwanaume.
Hata
hivyo, anasema suala la kuolewa lilimshtua sana , likamnyima raha sana
na kumtoa machozi. Anaeleza kuwa alitafakari na kuanza kusaka mbinu za
kujiokoa kwa kumfuata mama yake mzazi na kumwambia kuwa hataki kuolewa
na badala yake anataka kuendelea na masomo na ndipo alipohakikishwa na
mama yake kuwa atafanya kila njia ili kuhakikisha anasoma.
Anasema
wiki moja baadaye wakati akijiandaa kwenda shule asubuhi alibaini
kwamba sare zake na daftari zilikuwa zimefichwa na alipomwuliza mama
yake alimwambia kuwa baba yake ndiye aliyezificha kwa sababu hataki
kusikia yeye akiendelea kusoma.
“Nilishindwa hata kufanya
mtihani wa darasa la sita wa kwenda la saba kwa sababu sare zangu
zilifichwa , nikaenda kutoa taarifa kwa mwalimu mkuu,lakini baadaye baba
akaniambia kuwa hata mwalimu hatanisaidia lolote kwani ameshamalizana
naye,” anasimulia.
Anaeleza kuwa jambo hilo lilimumiza sana
kichwa akaamu kumfuata ofisa elimu wa Wilaya ya Kilindi na kumshitaki
mzazi wake, lakini kwa sababu likizo ilikuwa imeanza alimtaka afanye
subira hadi zifunguliwe shule mwezi Januari mwaka huu.
“Ilipofika
Januari na shule zilipofunguliwa nilimfuata tena ofisa elimu, kisha
nikaenda kituo cha polisi, lakini baba alipoitwa na kuhojiwa, hali
kwangu ilikuwa mbaya zaidi nyumbani kwani alisema nitamkoma kwa sababu
nataka kumfunga na kwamba sitafanikiwa, nitaolewa tu.”
Anasema
kuwa mambo yalipozidi kuwa magumu kwake aliamua kukimbilia kwa diwani wa
Kata ya Masagaru kuomba maskani kwani alihisi maisha yake yalikuwa
hatarini.
Binti huyo anaongeza kuwa hayuko tayari kuolewa kwa
sasa bali kiu yake ni kusoma hadi kiwango cha chuo kikuu ili apate kazi
itakayomsaidia kuwalea wazazi wake pamoja na wadogo zake kwa sababu
familia yake inaishi maisha duni.
Anaongeza kuwa haamini kama
kweli mahari ya ng’ombe watano iliyotolewa ili aolewe kama itawaweza
kuwakwamua wazazi wake kwenye maisha duni bali anachoamini yeye ni kuwa
kwa wakati huu elimu pekee ndiyo mkombozi.
“Nimeapa! Siko tayari
kuolewa nataka kusoma hadi chuo kikuu ili nipate kazi nzuri ambayo
itaniwezesha kuisaidia familia yangu ambayo inaishi maisha duni na
siamini kama ng’ombe watano watasaidia,kama ni ng’ombe nitanunua
nikianza kujitegemea nikiwa na kazi yangu,”anasema.
Naye diwani
(Makengwa) anakiri kumpokea mwanafunzi huyo na kusisitiza kuwa
atahakikisha binti huyo ambaye amekuwa mkimbizi kwake atasoma kwa njia
yoyote kwa kuwa ni haki yake ya msingi.
Anaongeza kuwa yeye kama mwakilishi wa wananchi hawezi kuona wanafunzi wasichana wakiachishwa masomo ili waolewe.
“Baba
yake anatumia fedha kuzinyamazisha mamlaka husika ili zisichuke hatua
hatimaye binti huyu aolewe, lakini kwetu amekwama kwani mimi, ofisa
elimu wa wilaya pamoja na mwalimu mkuu wa shule ya Kingo tumekaa imara
kuhakikisha binti hyuyo (Ngaisi) haachishwi masomo yake,”anasema diwani .
Mwalimu
mkuu wa shule hiyo, Juma Bwaki anasema amefanya kila njia kuhakikisha
mwanafunzi huyo hakatishwi masomo kwani amewezesha kupatikana kwa namba
yake ya kufanyia mtihani wa taifa wa darasa la saba mwishoni mwa mwaka
huu ambayo ni nambari 026 .
Ofisa Elimu wa Wilaya ya Kilindi,
Gideon Mwesiga anasema tatizo la mwanafunzi huyo kutaka kukatishwa
masomo lilianza tangu mwaka jana, lakini jitihada za kumnusuru
zinaendelea kufanyiika kwa kutumia vyombo vya dola na vya sheria.
“Binti
huyu ni mwanfaunzi anastahili sifa na kwa kweli anahitaji kuendelezwa
kwani maendeleo yake kitaaluma ni mazuri, lakini ikizingatiwa kuwa
anatoka familia ya wafugaji amefanya ujasiri wa hali ya juu kulifichua
suala hili”anasema Mwesiga.
No comments:
Post a Comment