Hali hiyo imedhihirika kufuatia madaktari katika hospitali mbalimbali nchini kujitokeza hadharani na kutangaza azma yao ya kugoma keshokutwa kuishinikiza serikali kutekeleza madai yao.
Wasiwasi wa kufanyika mgomo huo unakolezwa na kimya cha serikali ambayo licha ya madaktari hao kutangaza azma yao ya kugoma, hadi kufikia jana serikali ilikuwa bado haijatoa taarifa yoyote kuhusiana na hatima ya utekelezaji wa madai ya madaktari.
Akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alisema kufikia jana walikuwa hawajapokea taaraifa yoyote kutoka serikalini kuhusiana na madai yao.
Dk. Ulimboka alisema kuwa leo wanatarajia kutoa tamko kuhusiana na suala hilo.
Wakati madaktari wakijianda kugoma, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, amesema kuwa serikali inasubiri maamuzi ya Tume ya Usuluhishi kwa kuwa suala hilo liko katika mkondo wa sheria.
Akizungumza na NIPASHE jana jioni, Dk. Mwinyi alisema serikali haiwezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa inasubiri sheria ifuate mkondo wake.
Alisema wakati wa mgomo wa kwanza, suala hilo lilifikishwa mahakamani na mahakama kuamua liende katika Tume ya Usuluhishi ambayo ilitoa muda kwa serikali na madaktari kujadiliana ili kufikia mwafaka.
Alisema juzi Tume hiyo ilitakiwa kufuatilia makubaliano, lakini madaktari walikwenda katika Tume na kusema kuwa hawajakubaliana na serikali.
Hata hivyo, alisema kati ya madai 10 ya madaktari, matano yamekelezwa. Moja ya madai hayo alisema ni kuongezwa kwa posho ya kuitwa kazini kutoka Sh. 10,000 hadi Sh. 25,000.
Posho nyingine ni posho ya uchunguzi wa maiti kutoka Sh. 10,000 hadi Sh. 100,000 kwa daktari bingwa na wasaidizi wake Sh. 50,000. Nyingine ni kupewa kadi ya kijani kwa ajili ya huduma za afya na kupewa chanjo ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza.
Dk. Mwinyi alisema dai lingine la kutaka uongozi wa wizara kubadilishwa limeshatekelezwa.
Hivi karibuni, madaktari waliipa serikali wiki mbili kuhakikisha inatekeleza madai yao, vinginevyo watagoma tena kama mgomo wa Januari na Fenruari mwaka huu uliotikisa sekta ya afya na kusababisha madhara makubwa kwa wagonjwa katika hospitali nyingi za umma.
Pia hawakukubaliana na maelezo ya ripoti ya kamati ya serikali iliyopewa kazi ya kushughulikia madai ya madaktari.
Walisema ripoti hiyo imeshindwa kueleza jinsi madai yao yatakavyoshughulikiwa, likiwamo la nyongeza ya mshahara, ambapo walitaka kima cha chini kiwe Sh. milion 3.5.
Walidai wamegundua katika ripoti hiyo kuwa serikali haina nia ya kutekeleza madai yao na kwamba kila wanapokutana katika kikao, wamekuwa wakijibiwa majibu yasiyoridhisha.
Walisema kuna madai yao, ambayo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyatolea maamuzi walipokutana katika mkutano uliowakutanisha madaktari wote katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambayo kamati hiyo imeyaondoa wakati yalishafanyiwa kazi.
Walisema Pinda aliwaambia katika kipindi cha bajeti ijayo kuhusiana na posho ya madaktari kwa wale wanaoitwa kuendelea na kazi wakati wanapokuwa katika mapunziko walijulishwa kuwa daktari bingwa atapatiwa Sh. 50,000 na kwa daktari wa kawaida atapatiwa Sh. 40,000. Hata hivyo, walisema suala hilo limeondolewa.
Madaktari hao walisema katika suala hilo kamati imeamua kuondoa utekelezaji huo na kubakiza Sh. 20,000 na Sh. 25,000 kwa daktari bingwa, wakati Waziri Mkuu aliziongeza kwa kiwango hicho na kuwaahidi kuwa katika bajeti ya mwaka 2012/2013 wataongezewa kiwango hicho.
Mbali na hayo, pia walisema kuna mambo mbalimbali ambayo kamati hiyo imeshindwa kuwatekelezea licha ya kwamba waliahidiwa kuwa yangefanyiwa kazi na serikali.
Kutokana na hilo, madaktari waliipa serikali siku 14 kuhakikisha inatekeleza madai yao na kwamba kama haitafanya hivyo wanajianda kufanya mgomo wa madaktari wote nchini.
Pamoja na hilo pia walitangaza mgogoro baina yao na serikali.
KCMC WATANGAZA MGOMO
Wakati Ulimboka akisema hivyo, madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro jana walitangaza kujiunga na mgomo huo iwapo serikali itashindwa kutoa majibu ya madai yao.
Mwenyekiti wa madaktari hao, Dk. Rosemary Mrina, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Juni 15, mwaka huu, walikutana na kujadili kwa kina taarifa ya serikali ya kamati ya majadiliano baina ya serikali na madaktari iliyoundwa wakati wa mgomo wa awali.
Dk. Mrina alisema hawajaridhishwa na majibu ya serikali kwani yameshindwa kuwa na jibu la kutatua kero zao.
Kero hizo ni upungufu wa vifaa tiba na dawa, mazingira magumu ya kufanyia kazi, maslahi yao ikiwemo posho mbalimbali ambazo ni stahili zao.
Daktari Mugisha Nkoronko ambaye ni mjumbe wa kamati ya kitaifa ya kushughulikia madai ya madaktari alisema tayari Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimetangaza mgogoro wa wiki mbili kati yake na serikali, hivyo ni wazi kuwa watakaoathirika ni wananchi.
“Hatupendi ile hali ya wakati ule ijirudie, lakini serikali inatulazimu kufika huko kutokana na majibu mapesi yaliyotolewa, tumepeleka madai ya kurasa 50 wamejibu kwenye karatasi moja, moja ya maadui watatu tunaopigana nao tangu nchi ipate uhuru ni maradhi, lakini serikali imeshindwa kutatua kero zetu ili nasi tufanye kazi katika mazingira mazuri,” alisema.
Alisema madai ya madaktari yamebebwa na hoja nzuri na za msingi, lakini majibu ya serikali ni mepesi sana na ambayo huwezi kuyatarajia na kuwa mgogoro huo ulishafika kwa rais ambaye aliingilia kati na kuahidi kuutatua, lakini hakuna lililofanyika.
Dk. Anette Kessy alisema serikali imewapuuza wakati mgogoro uliopita Rais Jakaya Kikwete aliahidi kuupatia suluhu, lakini hadi sasa hakuna majibu waliyoyapata.
Juzi madaktari katika Hospitali ya Rufani ya Bugando jijini Mwanza walitangaza kuunga mkono mgomo huo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment