KAZI YAKE KUTAFUTA VYANZO VIPYA VYA MAPATO, KUONGEZA BAJETI YA MAENDELEO
WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda ameunda Kamati Maalum ya mawaziri sita kusaidia
mchakato wa marekebisho ya Bajeti ya Serikali ambayo mjadala wake
utahitimishwa kesho.Kuundwa kwa kamati hiyo kunazifanya kamati
zinazoifanyia kazi Bajeti ya 2012/2013 kufikia tatu.
Ijumaa
iliyopita wabunge wa CCM waliunda kamati ndogo kwa ajili ya kusaidi
pamoja na mambo mengine kuangalia vyanzo vingine vya mapato na kuona
iwapo bajeti ya maendeleo inaweza kuongezwa, kukidhi kiu ya wabunge.
Kamati
nyingine ni ile ya Fedha na Uchumi ya Bunge ambayo tayari imetoa maoni
yake bungeni kuhusu Bajeti, lakini ikabainisha kuwapo kwa kasoro kadhaa
ambazo zinapaswa kurekebishwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alikiri kuundwa kwa kamati
hiyo, lakini akakataa kutoa taarifa za kina kuhusu suala hilo kwa
maelezo kwamba huo ni utendaji wa kawaida wa shughuli za Serikali.
“Sidhani
kama hiyo ni habari kubwa ya kwenda kwenye public (kwa umma). Kwanza
siyo kamati ya mawaziri, haiwezi kuwa hivyo, na huo ni utendaji wa
kawaida wa ndani ya Serikali maana sisi tuna mambo mengi
tunafanya,”alisema Lukuvi na kuongeza:
“Kamati za utekelezaji wa
shughuli za Serikali ziko nyingi sana na siyo tu za Bajeti. Kwa hiyo
ndio maana nakwambia hilo ni jambo dogo sana ambalo mimi sidhani kama
linahitaji kutangazwa, kama lingekuwa hivyo mimi ningekuwa wa kwanza
kutaka kulizungumzia,” alisema.
Kazi ya Kamati
Habari
ambazo Mwananchi limezipata zinasema kwamba kamati ya mawaziri nayo
inafanya kazi ya kubuni vyanzo vingine vya mapato ya Serikali, ili
kufidia pengo la baadhi ya kodi ambazo zinatarajiwa kufutwa kutokana na
shinikizo la wabunge.
Miongoni wa kodi hizo ambazo huenda
zikafutwa wakati Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa atakapohitimisha
Bajeti yake kesho, ni ile inayopendekezwa kuongezwa kwenye muda wa
maongezi ya simu na ile ya inayopendekezwa kutozwa kwa waendesha
pikipiki maarufu kama bodaboda.
Kadhalika, kamati hiyo ya
mawaziri imepewa jukumu la kuona iwapo itaweza kushauri uwezekano wa
kuongezwa Bajeti ya sasa ya maendeleo kutoka asilimia 30 inayopendekezwa
na Serikali, jambo ambalo pia limekuwa likipigiwa kelele na wabunge
wengi.
“Hatuwezi kufumua Bajeti nzima ila kusema kweli ni kwamba
lazima kutakuwa na mabadiliko mengi, tatizo kubwa ambalo linatuumiza
vichwa, tunajiuliza kama tunaweza kupata hiyo nyongeza ya hizo fedha za
maendeleo walau Sh500 bilioni,”alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Taarifa
zaidi zimewataja wajumbe wanaounda kamati hiyo ambayo ilifanya kikao
chake cha kwanza juzi kuwa ni Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Mgimwa,
Lukuvi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Wengine
katika kamati hiyo iliyoundwa kwenye kikao cha kazi cha Baraza la
Mawaziri, Jumamosi iliyopita chini ya Pinda, ni Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa
Chakula, Kilimo na Ushirika, Adam Malima na Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima.
Habari zaidi zilidai kuwa
mawaziri hao watafanya kazi hiyo sasa na hata baada ya Bunge la Bajeti
ili ushauri wao uweze kuzingatiwa katika maandalizi ya bajeti ijayo ya
2013/2014.
“Tunawatarajia kwamba watatusaidia hata katika bajeti za kisekta zinazokuja,” alisema mjumbe mwingine wa kikao hicho.
Wasiwasi
ulikuwa ni iwapo ushauri wa kamati hiyo utaweza kuzingatiwa katika
majumuisho ya Waziri wa Fedha na Uchumi wakati atakapohitimisha Bajeti
yake, lakini jana Spika wa Bunge, Anne Makinda alifungua milango
inayowezesha Serikali kuongeza vyanzo vipya vya mapato hata baada ya
Bajeti Kuu kupitishwa.
Uamuzi wa Bunge
Jana Spika Makinda
alisema Bunge limeahirisha kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria za
Fedha wa mwaka huu, na sasa muswada huo utapitishwa mwishoni kabisa mwa
Mkutano wa nane Bunge.
Hatua hiyo ni dalili kwamba Serikali sasa
iko tayari kufanya marekebisho makubwa ya Bajeti yake na hata zile za
kisekta, hasa katika maeneo ya kuongeza vyanzo vipya vya mapato kadri
Kamati za Bunge, wabunge na Kambi ya Upinzani watakavyopendekeza.
Kusogezwa
huko pia kumewezesha kuongezwa siku moja ya majadiliano ya hotuba ya
Bajeti kutoka siku nne hadi tano, pia unatoa fursa ya Serikali kuongeza
vyanzo vyake vya mapato kwa kuzingatia maoni, mawazo na ushauri wa
wabunge.
Muswada wa Sheria ya Fedha ulikuwa umepangwa
kuwasilishwa kesho kama hitimisho la mjadala wa Bajeti ya Serikali,
lakini sasa umepelekwa mbele kutokana na kile Makinda alichosema kuwa ni
kutoa fursa kwa wabunge kuishauri Serikali kuhusu vyanzo vipya vya
mapato.
Makinda alisema uamuzi huo ulifanywa katika kikao cha
Kamati ya Uongozi cha Juni 18, mwaka huu baada ya kuzingatia maoni ya
wabunge, Serikali na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ambao walitaka
kuahirishwa kwake, ili kuruhusu Serikali kuongeza vyanzo vya mapato
kadri itakavyoshauriwa na wabunge.
Aliongeza kuwa Bunge
limeridhika kwamba licha ya kutopitishwa kwa muswada huo mapema kama
inavyotakiwa, bado Serikali itaweza kukusanya kodi kwa kutumia sheria
nyingine za nchi zilizopo.
Mabadiliko hayo ni mwanzo wa mchakato
wa mabadiliko ya Kanuni za Bunge ili kuwezesha vikao vya Bunge la
Bajeti kufanyika mapema na kuhitimishwa Juni 30, ili kuruhusu Serikali
kuanza mwaka wa fedha baada ya Bajeti nzima na Sheria ya Fedha kuwa
vimepitishwa.
“Mabunge mengi ya Jumuiya ya Madola yana utaratibu
wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha na Muswada wa Mutumizi mwishoni
kabisa mwa mjadala wa Bajeti. Lakini tumefuatilia na kubaini kuwa
mchakato wa kupitia Bajeti ya Serikali huanza mapema na kumalizika kabla
ya mwaka mpya wa fedha kuanza,”alisema Makinda na kuongeza:
“Bunge
letu lingepaswa liwe linakutana na kuanza mchakato wa kupitia Bajeti ya
Serikali mapema, ili inapofika Juni 30, mkutano wa Bajeti uwe
umemalizika na Muswada wa Sheria ya Fedha kuanza kutumika ifikapo Julai
Mosi ambapo mwaka mpya wa fedha unaanza”.
Alisema kutokana na
hali hiyo Kanuni za Bunge zitaendelea kufanyiwa marekebisho ili mikutano
ya Bunge la Bajeti iweze kuanza mapema kama ilivyo katika nchi nyingine
za Jumuiya ya Madola.
Kwa upande Lukuvi, alisema uamuzi wa
Serikali kukubali hoja ya kusogezwa mbele muswada huo, ni kutoa fursa ya
kuzingatiwa kwa maoni ya wabunge na kuendelea kuibuliwa kwa vyanzo
vipya vya mapato.
“Kama Serikali isingekubali, basi ujue hilo la
kuahirisha muswada lisingewezekana kabisa, maana ukishapitisha Muswada
wa Sheria ya Fedha hata maoni yatakayoendelea kutolewa kwenye bajeti
nyingine yangekuwa hayana maana,” alisema Lukuvi.
Mbunge alipua mawaziri
MBUNGE
wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), amewataka wabunge kumsaidia Rais Jakaya
Kikwete kuikataa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13, kwa kuwa mawaziri
wake wameshindwa kumsaidia kuleta Bajeti ambayo inajibu matatizo ya
Watanzania.
Alitoa kauli hiyo wakati akichangia kwenye mjadala wa
Bajeti na baadaye kutoa ufafanuzi wa kauli yake nje ya Bunge, kuwa
mawaziri wa Kikwete wameshindwa kumsaidia, kwani wametenga fedha nyingi
katika matumizi mengineyo na kutelekeza mpango wa Serikali wa Miaka
Mitano.
Neville Meena na Mussa Juma, Mwananchi- Dodoma
No comments:
Post a Comment