SERIKALI ya Kenya imesema inazifanyia kazi taarifa za raia wake
kukamatwa na kufikishwa kortini nchini kwa tuhuma za kumteka na kufanya
jaribio la kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven
Ulimboka.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Jeshi la Polisi
kutangaza kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa raia wa Kenya, Joshua
Mulundi anayetuhumiwa kuhusika na tukio la kumteka, kumpiga na kumtupa
Dk Ulimboka katika Pori la Akiba la Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam hivi karibuni.
Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso,
alisema kwa njia ya simu jijini Dar es Salaam jana kuwa Serikali yake
itachunguza uraia na tuhuma zinazomkabili mtu huyo ili kubaini ukweli.
“Ndiyo
kwanza nimewasili kutoka nje ya nchi…, nitafuatilia kwa makini kupata
taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo sahihi na mamlaka husika za hapa
Tanzania na Kenya ili kupata taarifa ya kweli,” alisema Balozi Mutiso na
kuongeza: “Siwezi kueleza zaidi kwa sasa kwani itakuwa naeleza uvumi.”
MAT wadai kutoridhishwa
Wakati
Balozi wa Kenya akisema hayo, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT),
kimeelezea kutoridhishwa na hatua hiyo kikisisitiza msimamo wake wa
kutaka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi kwa lengo la kuwabaini
wahusika na kuchukuliwa hatua stahiki.
MAT pia imesema kwamba,
inaendelea na mpango wake wa kuandamana, ikibainisha kuwa kesho
itawasilisha barua ya kuomba kibali cha kufanya maandamano ya amani
Polisi.
Imefafanua kuwa malengo ya maandamano hayo yaliyopigwa
'stop' na polisi kwa kile walichoeleza ni sababu mbalimbali za kiusalama
na kwamba, madai mengi ya madaktari yamefanyiwa kazi na Serikali.
"Nisingependa
kuingilia suala la kipolisi kwa ujumla wake, lakini moja ya madai yetu
ni kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza tukio la kutekwa, kupigwa na
kutupwa katika Msitu wa Pande kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk
Ulimboka," Katibu Mkuu wa (MAT) Dk Rodrick Kabangila aliliambia
Mwananchi Jumapili jana.
TUCTA nao wamo
Katika
hatua nyingine, Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (Tucta)
limelipongeza Jeshi la Polisi kwa kumkamata mtu anayedaiwa kumteka na
kumpiga kiongozi wa mgomo wa madaktari, Dk Steven Ulimboka.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema
kuwa, hatua ya kumkamata mtuhumiwa huyo inaleta matumaini ya kuwabaini
watu wengine waliohusika na vitendo hivyo, jambo ambalo linaweza
kurahisisha uchunguzi.
Alisema kutokana na hali hiyo, jeshi hilo
linatakiwa kuendelea na uchunguzi ili waweze kuwabaini wahusika wengine
na kubaini ukweli kuhusu tukio hilo ambalo limesababisha kutokea kwa
hisia tofauti katika jamii.
“Tunaliomba Jeshi la Polisi liendelee
na uchunguzi ili waweze kuwabaini watuhumiwa wengine na kuwachukulia
hatua za kisheria,” alisema Mgaya.
Mkenya kukamatwa
Joshua
Mulundi, ambaye anatuhumiwa kumteka na kumtesa Dk Ulimboka alikamatwa
na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini
Dar es Salaam juzi alasiri na kusomewa mashtaka mawili na Wakili wa
Serikali, Ladslaus Komanya.
Wakili Komanya alidai mahakamani hapo
kuwa, Mulundi ambaye makazi yake ni Murang'a nchini Kenya mnamo Juni
26, mwaka huu akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dk Ulimboka.
Hata hivyo, kumetokea utata wa jina, umri wake na makazi ya mtuhumiwa huyo.
Wakati
hati ya mashtaka mahakamani inasema ni Joshua Mulundi mwenye umri wa
miaka 21, mkazi wa Murang’a nchini Kenya, taarifa ya Jeshi la Polisi
imesema anaitwa Joshua Mahindi mwenye miaka 31 na mkazi wa Namanga
nchini Kenya.
Katika shtaka la pili, Wakili Komanya alidai kuwa
tarehe hiyohiyo mshtakiwa alifanya jaribio la kumsababishia kifo Dk
Ulimboka kwa kumpiga katika eneo la Msitu wa Pande eneo la Tegeta jijini
Dar es Salaam, kinyume cha sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo akidai kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo siyo sahihi.
Hakimu
Mkazi, Agnes Mchome alimwambia kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, isipokuwa
Mahakama Kuu pekee.
Afya ya Dk Ulimboka yazidi kuimarika
Akizungumzia
hali ya Afya ya Dk Ulimboka anayeendelea na matibabu nchini Afrika
Kusini, Katibu Mkuu huyo wa MAT alisema kuwa, Mwenyekiti huyo wa Jumuiya
ya Madaktari Tanzania anaendelea vizuri na sasa ameanza kufanya mazoezi
ya kutembea.
"Taarifa tulizonazo sasa ni kwamba, hali ya Dk
Ulimboka inaendelea vizuri. Ameanza kufanya mazoezi ya kutembea
mwenyewe, anakula na pia anaweza kuzungumza vizuri. Amekuwa akifanya
mawasiliano yeye mwenyewe na madaktari wenzake wa hapa nchini ingawa
bado kuna matibabu anayoendelea nayo," alisema Dk Kabangila.
Mmoja
wa Madaktari wa karibu wa Dk Ulimboka aliyepo nchini, alisema
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania amewatumia ujumbe wa
kuwashukuru wanataaluma wenzake na Watanzania wote waliomchangia na
kumwezesha kupata matibabu nchini humo.
Hata hivyo alisema kuwa,
Dk Ulimboka ameomba suala la tukio lake la kutekwa na kuumizwa lisiwe
hoja ya kujadili, badala yake madaktari na wananchi wote wajielekeze
kudai haki zao, ambazo Serikali haijazipa kipaumbele.
Dk Ulimboka
alisafirishwa nje ya nchi Juni 30 kwa ajili ya matibabu kufuatia jopo
la madaktari lililokuwa likimtibu likiongozwa na Profesa Joseph Kahamba
kudai afya yake imebadilika ghafla na pia angestahili kupelekwa nje ya
nchi kwa ajili ya vipimo na matibabu zaidi ambayo hayapatikani hapa
nchini.
CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment