MNADHIMU wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ameingia matatani
kutokana na kauli yake kwamba Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiteua majaji
wa Mahakama Kuu wasiopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Kutokana
na kauli hiyo aliyoitoa wakati akiwasilisha maoni ya kambi yake, kuhusu
hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria, Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) atajadiliwa na
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Wakati akisoma
hotuba yake, mbunge hiyo alisema majaji wanaoteuliwa na Rais hawafanyiwi
‘vetting’ (uchunguzi) na tume hiyo kuona kama uwezo na ujuzi wao unafaa
kukabidhiwa madaraka ya ujaji.
Mwenyekiti wa Bunge, Jenista
Mhagama ndiye aliyeamuru suala la Lissu kupelekwa katika kamati hiyo
baada ya mbunge huyo kukataa kufuta kauli yake ambayo kwa mtazamo wa
Serikali iliwadhalilisha majaji.
Hata hivyo, jana alipotakiwa
kueleza kama ana taarifa rasmi za kuitwa kwenye kamati hiyo Lissu
alisema: “Sijaitwa, lakini nina taarifa kuwa naweza kuitwa.’’
Alisema,
hata wakimwita hatakuwa na jambo lolote la kuzungumza kwa kuwa
Mwenyekiti wa Bunge aliyeongoza kikao hicho juzi (Jenista Mhagama),
alikosea kwa kuwa ndiye aliyepaswa kumpa adhabu.
Mbunge huyo
alisema juzi aligoma kufuta kauli yake kama alivyotakiwa na Mwenyekiti
kwani aliamini kuwa hata Mwanasheria Mkuu alikuwa amekosea.
Alibainisha
kuwa endapo ataitwa katika kamati hiyo, atahoji kama waliomwita
wamegeuka kuwa wenyeviti wa Bunge na kama si hivyo, anaamini watakosa
neno la kumhoji.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kwa nyakati tofauti
wakati wakijibu hoja za wabunge juzi jioni walisema: “Lissu aliwakashifu
majaji bungeni, hivyo alipaswa kuomba radhi.”
Kwa upande wake
Werema alimtaka Lissu kufuta kauli yake na kwamba ikiwa hatafanya hivyo
basi awasilishe vielelezo vinavyothibitisha madai kwamba majaji
huteuliwa bila kufanyiwa uchunguzi.
“Lissu ni mtaalamu wa
sheria, lakini kauli yake imewafedhehesha majaji na inashangaza
inapotolewa na wakili machachari kama yeye,” alisema Werema.
Werema
pia alimtaka Lissu kuondoa kauli yake kwa kuwataja watu ambao sio
wabunge kwa kunukuu gazeti la Mwanahalisi lililowataja watu watatu kuwa
wamehusika na mauaji ya Dk Steven Ulimboka.
Werema alisema iwapo Lissu hataondoa maneno yake suala hilo lipelekwe katika Kamati ya Maadili.
Kwa upande wake, Chikawe alimwombea radhi Lissu kwa majaji akisema anajua hakutoa kauli ya kuwadhalilisha majaji kwa kukusudia.
“Lissu
amemtuhumu hadi Rais katika uteuzi wa majaji, hili siyo sahihi, uteuzi
wa majaji hupendekezwa na tume maalumu inayohusisha majaji wazoefu ambao
ndio wanapendekeza majina kwa Rais,” alisema Chikawe.
Baada ya
maelezo hayo, Mhagama aliamuru Lissu kuondoa kauli yake hiyo baada ya
kutakiwa kufanya hivyo na Werema wakati akifanya majumuisho ya mjadala
wa wizara hiyo.
Hata hivyo, Lissu alipopewa nafasi alisema
hawezi kuondoa kauli yake kwa kuwa mchakato mzima wa kumtaka afanye
hivyo haukufuata Kanuni za Bunge.
Lissu alinukuu kanuni ya 63
(1) ambayo inasema: “Bila kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba
yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, ni
marufuku kabisa kusema uongo bungeni kwa sababu hiyo, mbunge yeyote
anapokuwa akisema bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli
au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni
kweli na siyo jambo la kubuni au la kubabaisha tu”.
Lissu
aliongeza kuwa, Jaji Werema na Mhagama walivunja Kanuni za Bunge kwa
kumtaka kuondoa kauli inayodaiwa kuwa ya uongo kinyume bila kufuata
utaratibu.
Alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa hatua hiyo jana,
Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema alisema kuwa siyo lazima kwa
Watanzania kufahamu hilo.
“Nilipozungumza jana (juzi) sikuzungumza
na Watanzania bali nilizungumza na Bunge, hivyo siyo lazima Watanzania
kufahamu jambo hilo na wala sioni sababu za kwa nini liandikwe
magazetini,’’ alisema Jaji Werema.
No comments:
Post a Comment