Saturday, July 7, 2012
Madaktari wakiri hali ya Ulimboka mbaya
Geofrey Nyang’oro na Zakhia Abdallah
UONGOZI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, umekiri kuwa hali ya Mwenyekiti wake, Dk Stephen Ulimboka ni mbaya na sasa amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), katika hospitali anakotibiwa huko Afrika Kusini.
Taarifa za Dk Ulimboka kuwa mahututi zilianza kupatikana juzi lakini hakuna daktari yeyote aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo baada ya kila aliyekuwa akiulizwa kueleza kuwa taarifa hizo zilikuwa uvumi tu.
“Asubuhi wote tulisikia kwamba hali yake (Dk Ulimboka) ni mbaya na yuko kwenye 'koma', lakini taarifa hizo sijazithibitisha kujua zina ukweli kiasi gani,” alisema Kiongozi wa jopo la madaktari linaloshughulikia matibabu ya Dk Ulimboka, Profesa Joseph Kahama juzi huku Katibu wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Rodrick Kabangila akisema alikuwa haelewi uvumi huo ulitoka wapi kwani yeye hakuwa na taarifa hizo.Rais wa MAT, Dk Namala Mkopi naye alikaririwa juzi akisema: “Bado sijawasiliana na Dk Ulimboka na hatujapata taarifa zozote za hali yake kama ni mbaya au vipi.”
Jana, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alithibitisha taarifa hizo na kueleza kuwa Dk Ulimboka yuko mahututi katika hospitali anakotibiwa huko Afrika Kusini.
Dk Ulimboka alisafirishwa nje ya nchi katikati ya wiki iliyopita baada ya jopo la madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lililokuwa likimtibu kutoa ripoti ya kubadilika ghafla kwa afya yake na kushauri asafirishwe nje kwa ajili ya vipimo na matibabu ambayo hayapatikani hapa nchini.
“Taarifa tulizonazo ni kuwa hali ya mgonjwa bado si nzuri na amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi,” alisema Dk Chitage.
Taarifa kuhusu Dk Ulimboka pia zilithibitishwa na Dk Mkopi akisema: “Kwa leo sijawasiliana na ndugu yake moja kwa moja, lakini habari nilizonazo ni kuwa hali yake bado siyo nzuri.”
Dk Mkopi alissema hali ya Dk Ulimboka haijatengemaa tangu juzi ilipobadilika... “Bado anapatiwa matibabu, lakini yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi na hali yake bado si ya kuridhisha.”
Katika hatua nyingine, madaktari wanaendelea kuchangishana kwa ajili ya matibabu ya Dk Ulimboka na katika awamu hii ya pili, imeelezwa kuwa takriban Dola za Marekani 30,000 zinahitajika.
Dk Mkopi alikiri madaktari hao kuendelea kuchangishana lakini hakuwa tayari kueleza kiasi ambacho kimepatikana mpaka sasa.
Madaktari wakosa ari
Upatikanaji wa huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), umezidi kuzorota huku baadhi ya madaktari wakisema tukio la Dk Ulimboka hilo limewapunguzia ari ya kufanya kazi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana kwa ombi la kutotajwa majina, baadhi ya madaktari wa Muhimbili, walisema tukio la kutekwa, kupigwa na kutupwa kwa Dk Ulimboka limewatisha.
“Kwa sasa madaktari hawana ari, hata wakifika eneo la kazi bado suala la kufanya kazi ni kitu kingine. Kitendo cha kutekwa kwa Dk Ulimboka kimetutisha sana, ” alisema mmoja wa madaktari wa Muhimbili.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwapo kwa baadhi ya madaktari bingwa katika MNH pamoja na Moi, ambao walithibitisha kuwa utendaji kazi hauwezi kuwa wa ufanisi kwa njia ya kulazimishwa.
“Serikali inachotakiwa siyo kulazimisha, inapaswa kusikiliza na kutatua hoja, sisi madai yetu yamepotoshwa, hatuna vifaa vya kufanyia kazi lakini wananchi hilo hawalielewi,” alisema mmoja wa madaktari hao.
Msemaji wa hospitali wa MNH, Eminael Aligaesha alisisitiza kuwa huduma katika hospitali hiyo zinarejea hatua kwa hatua... “Unajua tulikuwa katika kipindi kigumu lakini, niseme tu kuwa huduma zinazidi kuimarika siku hadi siku.”
Serikali yawashtaki
Serikali imewaandikia barua za kuwashtaki madaktari wote waliofukuzwa kazi kutokana na mgomo huo kwa Baraza la Madaktari Tanzania.
Katika barua hizo ambazo inadaiwa kuwa zimeshakabidhiwa kwa madaktari waliofukuzwa kutokana na mgomo, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imelitaka Baraza hilo kuchunguza na kuchukua hatua dhidi yao.
Baraza la Madaktari Tanzania ndilo lenye dhamana ya kusajili madaktari na ndilo lenye uwezo wa kutoa adhabu kwa madaktari hao ikiwa ni pamoja na kuwafutia usajili.
Sehemu ya barua hizo inasomeka, “Daktari mtajwa hapo juu alipelekwa katika Hospitali ya Taifa (MNH) kufanya mazoezi ya kuboresha taalamu kwa vitendo, tumepokea malalamiko kuwa kati ya Juni 23 na 29 mwaka huu alikataa kutoa huduma za kitaalamu ikiwa ni wajibu wake kama Daktari.”
“Kitendo hicho siyo tu kilihatarisha usalama wa wagonjwa walioletwa katika hospitali hiyo kwa matibabu, bali pia ni kinyume na maadili ya taaluma ya udaktari,” inasomeka barua hiyo iliyosainiwa na T.A. Chando kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara ya hiyo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment