Saturday, July 7, 2012

Ukimwi sasa kupimwa kwa mate

MAMLAKA ya Kudhibiti Chakula na Dawa Nchini Marekani (FDA), imethibitisha na kupitisha matumizi ya kifaa kipya cha kupima Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa kutumia mate.

Kifaa hicho kilichotengenezwa na wanasayansi wa nchini humo, kimeelezwa kuwa na uwezo wa kutoa majibu sahihi kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kati ya dakika 20 na 40 baada ya kupima.
Imeeleza kuwa kifaa hicho kilichopewa jina la OraQuick, kimebuniwa sio tu kwa ajili ya matumizi ya hospitalini bali pia nyumbani na kitaanza kupatikana katika maduka ya dawa nchini Marekani kuanzia Oktoba mwaka huu kabla ya kusambazwa nchi mbalimbali duniani.

Serikali ya Marekani imesema inaamini kifaa hicho kitasaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kubadili tabia ya watu wanaoishi na virusi hivyo bila kujua.
Wataalamu mbalimbali wa afya wamekielezea chombo hicho kuwa ni hatua nyingine kwa dunia katika jitihada zake za kudhibiti maambukizi ya VVU
.
Kinavyotumika
Kwa umbo OraQuick hakina tofauti na vipimo vingine vya kisasa ambavyo vimebuniwa kwa ajili ya kupima magonjwa kwa haraka kama vile malaria, Ukimwi na kisukari.
Lakini badala ya kuwa na sehemu ya kudondoshea tone la damu, kina sehemu laini iliyojitokeza, maalumu kwa ajili ya kunyonya mate.

Mtumiaji hapaswi kukitemea mate, bali kwa kutumia sehemu hiyo maalumu, atakiingiza kifaa hicho mdomoni na kuchukua mate katikati ya fizi na midomo chini au juu.

Sehemu hiyo laini italoa mate na kuyanyonya. Hapo mpimaji atapaswa kukiondoa kifaa hicho na kukiweka sehemu kavu kusubiri kimpatie majibu ndani ya muda huo wa kati ya dakika 20 na 40.

Gharama zake
Hakuna uhakika juu ya bei kamili ya kipimo hicho. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa kitauzwa kwa Dola za Marekani 17.50 sawa na Sh 27,300.

Taarifa zinaonyesha kuwa OraQuick itaanza kuuzwa Marekani na kusambazwa maeneo mbalimbali duniani na mtu yeyote ataweza kukiagiza kwa njia ya mtandao.

Moja ya masharti yaliyowekwa na FDA ni kwamba kipimo hicho kitauzwa kwa watu wenye umri wa miaka 17 au zaidi.

Kauli ya wataalamu
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID) Profesa Anthony Fauci alisema watafiti wa magonjwa wanaendelea kupiga hatua ya kudhibiti Ukimwi.
Alisema kipimo cha OraQuick ni moja ya hatua muhimu ambayo wanasayansi wamekuwa wakihangaika nayo usiku na mchana katika jitihada zao za kupata vipimo rahisi na tiba.

 Alisema jitihada za wanasayansi hao katika kupambana na Ukimwi zimewezesha kudhibiti maambukizi ya VVU kwa asilimia 96.

Daktari aliyegundua Mmarekani wa kwanza mwenye VVU mwaka 1984, Dk Robert Gallox alisema hatua ya FDA kupitisha kipimo hicho itasaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi hivyo duniani.

No comments:

Post a Comment