WAZIRI Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, jana
alifichua ufisadi katika sekta ya ardhi, huku akiilipua kampuni ya
kigeni iliyotumia leseni ya uwindaji,kuchimba madini.
Akiwasilisha
maoni ya kambi yake kuhusu hotuba ya makadirio ya Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mdee alisema kuna kila dalili kwamba
Tanzania imegeuzwa kuwa shamba la bibi kwa sababu kuna ukiukwaji mkubwa
wa sheria za nchi.
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema),
alisema mkataba baina ya kampuni ya Uranium Resourses PLC, Western
Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited, ni ushahidi wa
kuwapo kwa madudu mengi yanayofanyika huku Serikali ikiyafumbia macho.
Alisema
mkataba huo wa siri, umetengenezwa na Kampuni ya Uwakili ya Rex
Attorneys ulisainiwa Machi 3 mwaka 2007 na kwamba unaruhusu kampuni za
uwiandaji kufanya uchimbaji wa madini ya Uranium katika Kijiji cha
Mbarang’andu.
Mdee alisema Kampuni ya uwindaji ya Game Frontiers
of Tanzania Limited inayomilikiwa Mohsin M. Abdallah na Nargis M.
Abdallah, imeingia mkataba na kampuni mbili za kigeni zinazofanya
utafiti wa uchimbaji wa madini ya Uranium katika kijiji hicho.
Mdee
alisema mkataba huo ni wa malipo ya Dola 6 milioni za Marekani milioni
6 ambazo zitalipwa kwa awamu mbili ya malipo ya Dola 3 milioni kwa kila
awamu.
“Malipo ya kwanza yatafanyika pale uzalishaji wa Uranium utakapoanza.
Malipo
ya Dola 250,000, yatafanyika baada ya kampuni za madini kukamilisha
utafiti wa madini ya urani na kupata kibali cha uchimbaji wa
madini,”alisema Mdee.
Aliyataja malipo mengine kuwa ni Dola
55,000 za Marekani kila mwaka kama fidia ya kushindwa kufanya biashara
na usumbufu unaotokana na shughuli za machimbo kwenye kitalu na kwamba
malipo hayo yatafanyika kila Mach 31.
Mengine ni Dola 10,000 za
Marekani kwa vijiji vitakavyoathiriwa na utafiti huo wa urani, malipo
ambayo yametokana na makubaliano baina ya kampuni ya uwindaji na kampuni
za madini.
“Nimepitia sheria za uhifadhi wa wanyamapori, The
wildlife Conservation Act, 1974 (Sheria ya zamani) na Sheria mpya The
wildlife Conservation Act, Act no 5 of 2009. Sheria hizi zinamruhusu mtu
aliye na leseni ya uwindaji, kuwinda wanyama tu,”alisema Mdee na
kuongeza:
“Hali kadhalika, Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, Sheria
namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya vijiji, sheria namba 5 ya
mwaka 1999 inatamka bayana kwamba ardhi inajumuisha vitu vyote vilivyo
juu ya ardhi na chini ya ardhi isipokuwa madini au mafuta na gesi”.
Alihoji
sababu za kukikukwa kwa taratibu za nchi zinazoelekeza kwamba
linapokuja suala la madini, umiliki unatoka kwa mtu binafsi na kurudi
serikalini nakwamba Wizara ya Nishati na Madini ndiyo pekee yenye
mamlaka ya kutoa leseni ya kutafuta madini kwa kampuni za madini!
“Kambi
ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge lako tukufu uhalali wa
mkataba kati ya Game Frontiers na Uranium Resourses PLC na Western
Metals! Ni sheria ipi inayoipa kampuni ya uwindaji haki ya kualika
kampuni ya nje kwenye eneo ambalo haina umiliki kufanya utafiti na
hatimaye kuchimba madini hatari kama urani,,”alihoji.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment