Sunday, August 12, 2012

Mkapa amvuruga Kikwete

 - Kesi ya Mahalu yaibua uadui wa kisiasa

UAMUZI wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam uliomwachia huru aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Prof. Costa Mahalu, umeacha doa kubwa ndani ya serikali ya awamu ya nne, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.

Makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao hawakupenda majina yao yaandikwe wamedai kuwa chuki za wanamtandao dhidi ya kundi la wapinzani wao ndio kiini cha kushitakiwa na kufikishwa mahakamani kwa baadhi ya watu.

Wamedokeza kuwa, pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), Elieza Feleshi kukataa kuzipeleka baadhi ya kesi mahakamani, zilizoonekana kuwa za kukomoana, kulipizina visasi, bado kuna nguvu kubwa ya kushinikiza vigogo wa CCM na serikali waburuzwe mahakamani licha ya ushahidi kuonekana hafifu.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, huku ikiwaacha huru Profesa Mahalu na Grace Martin umeibua hisia nzito kutoka kwa wanaharakati na mabingwa wa uchambuzi wa masuala ya siasa kuwa, ndani ya kesi nyingi zilizofunguliwa mahakamani dhidi ya watendaji wa serikali, mawaziri, makatibu wakuu wa wizara ni za kisiasa.

Indaiwa ndani ya kesi nyingi zilizopewa nguvu ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka zinausishwa moja kwa moja na kundi la wanamtandao, ambao kwa kiasi kikubwa ndilo linalodaiwa limemeza mamlaka makubwa yanayopaswa kufanywa na serikali.

Kundi hilo ndilo linalodaiwa liliendesha harakati za kumhusisha Rais mstaafu Benjamin Mkapa na ufisadi uliofanywa katika utawala wake, kwa kutumia vyombo vya habari nchini ili kuujengea utawala wa Rais Jakaya Kikwete taswira nzuri mbele ya jamii.

Wachambuzi wa masuala ya sheria wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa, kitendo cha Mkapa kupanda kizimbani kumtetea Mahalu Mei 7, mwaka huu kilimaanisha mgawanyiko mkubwa ndani ya serikali.
Wataalamu wa sheria walibainisha kuwa, kesi ya Mahalu ilionesha udhaifu mkubwa kwa serikali, kwani Jamhuri ilikuwa inapambana na Jamhuri (Mkapa na Mahalu) na mashahidi wakawa Jamhuri.

Waliweka wazi kuwa licha ya Mkapa kuondoka madarakani, lakini bado ni kiongozi wa nchi na wakati wa uamuzi wa kununua jengo hilo, Rais Kikwete pia alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Tuhuma zilizomkabili Balozi Mahalu ni tuhuma za ununuzi usio sawa wa nyumba ya ofisi ya ubalozi wa Tanzania huko Italia. Tukio hilo lilifanyika wakati Mkapa akiwa rais wa Tanzania na Kikwete alikuwa waziri katika serikali hiyo hiyo.

Wanasheria hao wanaweka bayana kuwa, Mkapa alitoa ushahidi wenye maudhui ya kuthibitisha kwamba kilichofanyika chini ya utawala wake kilikuwa sahihi, na hivyo kutoa taswira kuwa utawala wa sasa ulikuwa ukifanya kitu kitakachoiumiza serikali na chama tawala kilichokaa madarakani tangu kupata uhuru.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaweka bayana kuwa, ushahidi wa Mkapa kwa kiasi kikubwa umechangia serikali kuanguka katika kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi.

Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa, baadhi ya vigogo wa CCM na serikali wameanza kuhofia kuwa kundi la wanamtandao wanaweza kuanza kuibua upya tuhuma za kiongozi huyo mstaafu ikiwa ni ishara ya kulipa kisasi.

Hata hivyo, mtandao huo ulioundwa kabla ya mwaka 2005 kwa lengo la kumsaidia Rais Kikwete kuingia madarakani, hivi sasa umegawanyika ambapo miongoni mwa waanzilishi wake wanatuhumiwa kwa ufisadi.

Miongoni mwa waanzilishi hao ni aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, aliyelazimika kujiuzulu ubunge wake kwa kile alichokiita siasa uchwara ndani ya chama chake baada ya kuhusishwa na tuhuma za ufisadi mara kwa mara.

Kinara mwingine wa mtandao, ni mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye baada ya Kikwete kuingia madarakani, alipendekeza jina lake kuwa Waziri Mkuu ambaye hata hivyo alijiuzulu mwaka 2008 baada ya kuguswa na kashfa ya Richmond.

Lowassa mpaka sasa amekuwa akipambana na baadhi ya vigogo wa chama chake anaodai wamekuwa wakieneza siasa za chuki na kulipaka matope jina lake mbele ya jamii, chama chake na Rais Kikwete ambaye urafiki wao haukuanzia barabarani.

Wakati mapambano ya makundi yanayomuunga mkono Mkapa na Rais Kikwete yakionekana kujipanga kusulubiana, CCM hivi sasa inakabiliwa na masuala mbalimbali, ikiwemo uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, chaguzi za jumuiya za chama na wajumbe wa vikao vya juu vya chama hicho.

Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa, mnyukano wa siasa za makundi hivi sasa huenda ukaathiri zaidi utendaji wa kazi ndani ya chama na serikali, ambapo baadhi ya watendaji wamekuwa wakifanya kazi kwa wasiwasi wakihofia kutoliudhi kundi mojawapo.

Mmoja wa wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu ambaye hakutaka kutajwa jina, alibainisha wazi kuwa kesi nyingi zilizopo mahakamani ni za kuwadhoofisha baadhi ya watendaji wa serikali, ambao ni wanasiasa walio nje ya mtandao ulioiwezesha serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani.

“Unajua ndugu yangu, mazingira ya kisiasa na tambo kubwa ziliibuka baada ya serikali ya awamu ya tatu ya Mkapa kumaliza muda wake, mambo mengi yaliibuka, huku kukiwa na kashfa nyingi zilizoanza kuibuliwa kuwa serikali hiyo haijafanya kitu na watendaji wengi kuvunjwa nguvu, miongoni ni wale waliokuwa ndani ya Baraza la Mawaziri la serikali ya Mkapa,” alisema.

Alisema kuwa haiwezekani kila kesi zinazopelekwa mahakamani serikali inashindwa, hivyo ni wazi kuwa hata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) haiwezi kutekeleza majukumu yake, kwa kuwa mhimili wa serikali umekuwa ukitoa fedha nyingi kutafuta ushahidi ambao mwisho wake watuhumiwa wanashinda.

Alibainisha wazi kuwa gharama nyingi zinazotumiwa na serikali ya awamu ya nne ili kuchunguza tuhuma zinazowabana watendaji wengi waliokuwa kwenye serikali ya awamu ya tatu ni kutokana na tofauti za kisiasa kwa kile kinachodaiwa kuwa wanatafunwa na msimamo wao wa kupinga kundi la mtandao katika harakati zake za kuchukua dola.

Ernest Mwansasu mkazi wa jijini Dar es Salaam akizungumza kwa njia ya simu, alisema kuwa utawala wa chuki, kulipizana visasi na hali ya kupeana madaraka kunachangia kwa kiasi kikubwa watu kuumizana kwa kesi za kubambikiana, huku wale waliothibitishwa kujihusisha na tuhuma za ubadhilifu wa mali za umma wakiachwa wakati hata mamlaka ya Bunge imekuwa ikiwatuhumu.

“Ebu angalia mambo haya, wengi wanaoumizwa hivi leo wanatolewa kafara, wako wapi walioiba fedha kupitia Kampuni ya Kagoda? Wako wapi watuhumiwa wa Richmond? Wako wapi watuhumiwa wa EPA? Wako wapi waliohusika kashfa ya rada? Hapa kuna siri nzito, huu wote ni mfumo unaolindana na kuwatoa kafara wachache,” alisema.

Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa ipo haja serikali ya CCM ikajitathimini upya kwa kuwa bado marais waliopita nao wana sauti ndani ya chama hicho, wana ujumbe wa heshima ndani ya vikao vya ngazi ya juu kichama.

CHANZO: TANZANIA DAIMA


No comments:

Post a Comment