Wednesday, October 17, 2012

Afya ya Spika yazua utata

KUNA taarifa za kutatanisha kuhusu afya ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambapo inadaiwa kuwa amelazwa katika Hospitali ya Apollo nchini India.

Habari za ambazo gazeti hili limezipata toka nchini India kwa watu wake wa karibu, zimeeleza kuwa Spika amelazwa tangu wiki iliyopita katika hospitali hiyo.

Vyanzo vyetu hivyo vilisema, Spika Makinda ameongozana na watu watano ambao wamekuwa wakionekana naye hospitalini hapo.
Hata hivyo, gazeti hili halikuweza kufahamu mara moja ugonjwa unaomsumbua kutokana na jambo hilo kuwa siri kati ya mgonjwa na madaktari wake.

Taarifa za ndani zinasema kuwa baadhi ya watu waliofika kumuona waliambiwa kwamba anasumbuliwa na macho.

Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, alikiri kuwa Spika alikwenda nchini humo kwa shughuli mbili ikiwamo ya kufanya uchunguzi wa afya wa kawaida.

Alisema Makinda alikwenda nchini humo mwanzoni mwa mwezi huu kwenye mkutano wa Maspika Wanawake (IPU) na baada ya kumaliza shughuli hiyo ndipo akaenda kufanya uangalizi wa afya yake.

Kashilila ambaye hata hivyo alikwepa kuzungumzia kama Spika amelazwa, aliishia kusema tu kwamba alipitia kufanya uangalizi wa kawaida wa afya yake na amekuwa akifanya hivyo kila mwaka.

Kwa mujibu wa Kashilila, Spika atarejea wiki ijayo baada ya kumaliza taratibu zote za kuangalia afya yake.

Wakati Dk. Kashilila akisema hivyo, mitandao mbalimbali ya intaneti, ilionyesha kuwa mkutano huo wa maspika wanawake ulifanyika kati ya Oktoba 3 hadi 4 mjini New Delhi, nchini humo.

Hivyo, endapo Spika alitoka kwenye mkutano na kupitia moja kwa moja kuangalia afya yake, atakuwa ametumia takriban siku 11 hadi kufikia leo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoandikwa kwenye mitandao ya intaneti, katika mkutano huo ambao mada kubwa iliyokuwa ikijadiliwa ni masuala ya jinsia, Spika Anne Makinda, alichangia kuhusu suala hilo akisema wanawake maspika wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba mabunge yanazingatia ujinsia.

Akichukulia mfano hatua ambazo Tanzania imechukua katika kufanikisha masuala ya kijinsia katika Bunge, Makinda alielezea umuhimu wa maspika wanawake kuhakikisha suala hilo linafanyika kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuanzisha kamati ya usawa wa kijinsia pamoja na suala zima la bajeti sanjari na kuimarisha muundo wa mabunge.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment