Wednesday, October 17, 2012

Watu 36 pamoja na mtoto anayedaiwa kukojolea kitabu kitakatifu cha Kur’an eneo la Mbagala, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na kesi nne tofauti ikiwamo kuchoma makanisa.

Mashitaka mengine waliyosomewa ni kuharibu mali zenye thamani ya Sh. milioni700 na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Katika kesi ya kwanza ya kuchoma makanisa, washtakiwa ni Mahenga Yusufu, Hamad Sokondo, Shego Mussa Abdallah Said, Ramadhani Salum, Mashaka Iman, Kasim Juma, Ibrahim Jumanne na Hamza Mohamed.

Wengine ni, Mikidad Sadik, Juma Mbegu, Rahib Abdallah, Issa Seleman, Hamis Kimwaga, Ramadhani Mbulu, Hemed Mohamed, Msham Alifa na Mohamed Yusufu.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo.

Upande wa mashtaka uliongoza na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumain Kweka, akisaidiana na Ladislaus Komanya.

Kweka alidai kuwa, Oktoba 10, mwaka huu eneo la Mbagala Zakhiem, wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Oktoba 12, mwaka huu katika eneo la Mbagala Zakhiem, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walivunja na kuingia ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) na kuharibu madhabahu yanayotumika kufanyia maombi na ibada kwa washarika wa kanisa hilo.



Wakili huyo alidai kuwa, siku ya tukio la pili, washtakiwa wote kwa makusudi waliharibu feni, milango, kiyoyozi, viti, mfumo wa umeme, makabati, makochi, madhabahu na uzio wa kanisa hilo vikiwa na thamani ya Sh. milioni 500.

Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa katika tukio la pili na la tatu, washtakiwa walifanya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha baada ya kuiba kompyuta mpakato (Laptop), kinanda, maspika na printa, vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 20 mali ya KKKT.

Ilidaiwa kuwa mara na kabla ya wizi huo, washtakiwa walimtishia kwa nondo na matofali mlinzi wa kanisa hilo, Michael Samuel, ili kujipatia mali hizo.

Katika shtala la tano, ilidaiwa kuwa siku ya tukio washtakiwa walichoma moto kanisa kwa makusudi mali ya KKKT Usharika wa Mbagala.

Katika kesi ya pili, kati ya Oktoba 10, mwaka huu washtakiwa wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la kuharibu mali.

Shataka la pili, ilidaiwa kuwa Oktoba 12, mwaka huu Mbagala Kizuiani, jijini Dar es Salaam, washtakiwa waliharibu vitu mbalimbali ikiwamo kuvunja milango, viti na madhabahu mali ya Kanisa la Anglikana Parokia ya Kizuiani.

Komanya alidai kuwa katika shtaka la tatu, siku ya tukio la pili, eneo la Mbagala Kizuiani, waliiba vitu mbalimbali mali ya kanisa hilo.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa katika kesi ya tatu, inawakabili washtakiwa Mwalimu Said, Omary Shaban, Ibrahim Msimbe, Abdallah Said, Pascal Kashiriri, Abdukadir Haji, Ahmad Juma na Mohamed Chobe kuwa Oktoba 12, mwaka huu huko Mbagala, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la uhalifu.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Oktoba 12, mwaka huu eneo la Maduka Tisa, Kibonde Maji, washtakiwa waliharibu vitu mbalimbali mali ya Kanisa la Agape vikiwa na thamani ya Sh. milioni 80.

Komanya alidai katika shtaka la tatu, Oktoba 12, mwaka huu, washtakiwa walichoma moto madhabahu sehemu inayotumika kwa ajili ya kufanya maombi kwa waumini wa Kanisa la Agape, mali ya kanisa hilo.

Katika kesi ya nne, washtakiwa ni Issa Abdallah, Hamisi Masudi, Ramadhani Mohammed, Hemedi Mohammed, Mshamu Alifa, Mohammed Musa, Hashimu Omary, Abas Saidi, Iddi Selemani, Yahaya Ngede, Daniel Ngamulile, Hassan Mohammed, Saidi Mkoba, Dodo Mohammed, Mohammed Hamisi, Amiri Mohammed na Ally Selemani.

Wakili huyo wa serikali alidai kuwa washtakiwa waliharibu magari mbalimbali likiwamo la Jeshi la Polisi.

Thamani ya magari ya Kanisa la TAG, SDA Usharika wa Mbagala thamani yake ni Sh.  56,790,000.

Pia, washitakiwa wanadaiwa kuvunja makanisa hayo na kuiba vifaa mbalimbali vya magari waliyoharibu, vyote vikiwa na thamani ya Sh 14,820,000.

Washtakiwa walikana mashtaka na mahakama ilisema itatoa masharti ya dhamana Oktoba 30, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, mtoto anayedaiwa kukojolea kitabu hicho kitakatifu alisomewa mashtaka katika Mahakama ya Watoto ya Kisutu.

Tofauti na siku nyingine panapokuwepo na kesi dhidi ya waumini wa Kiislamu, jana hali ilikuwa tofauti kwa sababu  viwanja vya mahakama  havikuwa na watu. Waliokuwepo ni ndugu wachache wa washtakiwa hao.

POLISI LAWAMANI


Askari polisi wamelalamikiwa kutokuwa makini kwao kulichangia athari za vurugu hizo.

Polisi wamedaiwa kushindwa kuwajibika baada ya kukaidi ushauri wa kulilinda kanisa la KKT Usharika wa Mbagala hata baada ya kupewa taarifa na waumini wa kanisa hilo kuwa baadhi ya watu walikuwa na kusudio la kulichoma.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo waliwaambia viongozi wa makanisa mbalimbali waliotembelea kanisa hilo jana kuwa polisi walitoa matamshi ya kukataa kutoa ulinzi muda mfupi kabla ya kuchomwa kwa kanisa hilo.

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao magazetini, walisema kuwa kanisa hilo lilichomwa na kundi la watu muda mfupi baada ya polisi kuondoka katika eneo la kanisa hilo.

Aidha, waumini hao walibainisha kuwa tukio hilo lilikuwa la kupangwa na halikufanywa na vibaka
kama baadhi ya watu wanavyodai.

ASKOFU MALASUSA ANENA

Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa, alisema kilichofanyika ni maangamizi kwani kama mtu angekuwa ndani ya kanisa angeweza kufa.

Askofu Malasusa ambaye pia ni Askofu wa KKKT Jimbo la Mashariki na Pwani, alisema kuwa waliangalia makanisa yote yaliyoathirika na watafanya tathmini ya vitu vilivyoharibiwa na watatoa tamko.

MAPALALA ATAKA MAZUNGUMZO


Mwenyekiti wa Chama cha Haki na Ustawi (Chausta), James Mapalala, ameiomba serikali kuitisha meza ya mazungumzo kati ya viongozi wa Kiislamu na Wakristo ili kuangalia namna ya kutatua tofauti  zinazojitokeza.

“Naiomba serikali isilale usingizi na kulifumbia macho tukio za vurugu zinazotokea kati ya Waislamu na Wakristo, ni lazima serikali itoe msimamo ili kuhakikisha amani kati ya pande hizo inarejeshwa,” alisema jana jijini Dar es Salaam wakati wa kufunguzi wa Mkutano Mkuu wa chama hicho.

Aliongeza: “Endapo serikali itanyamaza na kulipuuzia jambo hili kutatokea umwagaji wa damu na itakuwa imebeba mzigo wa dhambi.”

Alisema ifahamike kwamba dini zote zipo chini ya serikali moja na hakuna inayoweza kuitawala nyingine, hivyo hakuna haja ya kueneza chuki zinazoweza kusababisha kupigana.

“Nawaomba pia wale wanaotaka kupigana kwa ajili ya dini wafanye mazungumzo kumaliza chuki zao bila hivyo wanaweza kusababisha madhara,” alisema.

“Tumekuwa tukiona matatizo haya yakitokea katika nchi za wenzetu na kuzua madhara makubwa, hivyo na serikali yetu ikiyapuuzia yanaweza kusababisha matatatizo makubwa,” aliongeza.

PONDA AIBUKA


Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania imetoa siku saba kwamba katika muda huo Waislamu wanao shikiliwa na Polisi wapewe haki yao ya dhamana.

Taarifa hiyo imetolewa jana jijini Dara es Salaam na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Ponda Issa Ponda, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio la kuidhalilisha Kur’an.

Ponda alisema dhamana ni haki ya kila Mtanzania, hivyo kitendo cha Waislamu hao kunyimwa dhamana ni sawa na kuwanyima haki yao kisheria.

Ponda  pia alisema kuwa wanakemea vitendo vya uchochezi wa kidini, matumizi ya nguvu kubwa dhidi ya raia yaliyofanywa na polisi pamoja na baadhi ya viongozi kutumia madaraka kwa  kuwagawa Watanzania kwa misingi ya kidini.

Imeandikwa na Hellen Mwango, Elizabeth Zaya, Rehema Kilagwa na Jacqueline Yeuda.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment