Friday, May 31, 2013

Dawa za ARV zauzwa mitaani huko Rorya

Rorya. 

Imebainika kuwa dawa za kurefusha maisha kwa waathirika wa Ukimwi (ARVs) zinazotolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara, zimezagaa mitaani kwa kuuzwa kwenye maduka binafsi na yanayomilikiwa na watumishi wa vituo vya afya vya Serikali.


Akizungumnza katika kikao cha Baraza la Madiwani wilayani Rorya, Diwani wa Kata ya Mirare, Peter Ayoyi (CCM), alisema uzagaaji wa dawa hizo ulibainika baada ya halmashauri kufanya msako wa dawa za Serikali katika maduka binafsi ya kuuza dawa wilayani humo.

“Inasikitisha kuwa dawa za hospitali zinauzwa kwenye maduka binafsi hata wagonjwa wa Ukimwi wananunua dawa za kurefusha maisha kwenye maduka hayo, Naomba kujua? Inakuwaje dawa za Hospitali za Serikali zinauzwa au zinapatikana katika maduka ya mitaani?,” alihoji Ayoyi.


Akijibu swali la Ayoyi, Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji ambaye ni Diwani wa Kata ya Koryo, Peter Sarungi (CCM) alikiri kuwa ni kweli dawa za hospitali zikiwamo za kurefusha maisha zinauzwa katika maduka ya dawa yanayomilikiwa na watu binafsi.

Diwani Peter Ayoyi alimtaka Mganga Mkuu, Daniel Chacha na halmashauri ya wilaya kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki wa maduka yaliyokutwa yakiuza dawa za Serikali na za kurefusha maisha, kwa kuwa tangu ukaguzi huo ufanyike bado watu hao hawajachukuliwa hatua. 
   

No comments:

Post a Comment