Friday, May 31, 2013

Hoja ya ushoga yatikisa Bunge

Mbunge wa Nyamagana(Chadema), ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Ezekia Wenje, akitolewa nje ya Ukumbi wa Bunge na askari wa Bunge huku akionyesha alama ya ‘V’, baada ya wabunge wa CUF kutaka kumpiga, kutokana na hotuba yake waliyodai kuwaudhi wabunge hao. Picha na Emmanuel Herman. 


















Dodoma.

 Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai ameahirisha mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, baada ya msemaji wa kambi ya upinzani kwa wizara hiyo kukataa kuomba radhi kulingana na maagizo ya kiti cha Spika.

Ndugai alikuwa amemwamuru msemaji huyo wa Upinzani, Ezekiah Wenje aombe radhi kwa kile alichoeleza ni kukashifu chama cha CUF na afute maneno ya kashfa hizo kwenye hotuba yake.

Wenje alikubali kutosoma maneno hayo yaliyokuwa kwenye hotuba hiyo lakini akakataa kuomba radhi kwa maelezo kuwa yaliyoandikwa ni ya ukweli na ana ushahidi.

Awali wakati wa asubuhi pia Ndugai alilazimika kuahirisha kikao cha Bunge, baada ya kuzuka vurugu kubwa kati ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF).

Vurugu hizo zilizuka baada ya Mbunge wa CUF (Mtambile) Masoud Salim, kutoa hoja ya kutaka Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekiel Wenje, kusitisha hotuba yake kwa kile alichoeleza kuwa “imejaa uzushi, uhuni, uzandiki, uongo na ushenzi.”
Salim alitoa hoja hiyo saa 6:15 mchana, wakati Wenje akiwa anasoma hotuba hiyo katika ukurasa wa tatu.
“Mwongozo wa Spika,” alisema Salim muda mfupi kabla Naibu Spika Ndugai, hajampa fursa ya kutoa hoja yake.

Salim aliendelea: “Natoa hoja kwamba hotuba hii ni ya kizushi. Huu ni uhuni, uongo, ushenzi na uzandiki. Siyo ya kusomwa bungeni.”

Alitoa kauli hiyo akinukuu maneno yaliyoko kwenye ukurasa wa 8 wa kitabu cha hotuba hiyo yanayoeleza kuwa,”...Kwa upande wa CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga…’

Kipengele kilichowaudhi CUF kilisema hivi: “Hii ni kwa mujibu wa tangazo lao (CUF) kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa wa Uingereza, Lynn Featherstone kutoka chama cha Liberal Democrats wakati chama hicho kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu ndoa za jinsia moja kama haki ya mtu mmoja mmoja.

Salim alikiomba kiti cha Spika, kuamrisha Chadema waombe radhi, wafute kauli hiyo na Kamati ya Maadili iifanyie kazi taarifa yao kwa kuwa si ya kistaarabu.

“Kwanza wakome, wakome kwa asilimia 100. Wahuni hawa na tunataka wachukuliwe hatua za kinidhamu,” alisema Salim, huku akishangiliwa na Mbunge wa Nkasi (CCM), Ali Kessy ambaye aliibuka kitini na kuitikia,” Apigwe, apigwe, Msagaji mwenyewe (Wenje).”

CHANZO: GAZETI MWANANCHI


No comments:

Post a Comment