POLISI KUWAHOJI KWA MATAMSHI KWAMBA WANATISHIWA MAISHA, DK NCHIMBI ASEMA WANASABABISHA CHUKI
KATIBU
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na
Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema huenda wakajikuta
matatani kutokana na madai waliyoyatoa juzi kwamba wanatishiwa kuuawa na
kigogo mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa.Kutokana na matamshi hayo,
jana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi ameliagiza
Jeshi la Polisi kuwahoji viongozi hao ambao walidai kuwa mauaji hayo
yamepangwa kufanywa kwa kuwekewa sumu kwenye chakula au kwa kutumiwa
makundi ya ujambazi.
Akizungumza na waandishi wa mjini hapa jana,
Dk Nchimbi alisema licha ya kudai kwamba wanatishiwa, ameshangazwa na
msimamo wa viongozi hao kukataa kupeleka suala hilo polisi kwa madai ya
kuhofia suala hilo halitafanyiwa kazi.
Alisema watawahoji
viongozi hao kwa sababu suala la usalama wa Mtanzania yeyote si la
hiari, bali ni la kikatiba na la kisheria hivyo, ni lazima polisi
watimize wajibu wao.
“Ni lazima tuwahoji ili tujue ni nani
amewatisha na kwa sababu zipi. Hatutamuomba mtu ruhusa ya kumlinda kwa
sababu huo ni wajibu na kazi yetu kuwalinda raia, hilo halina mjadala.
Hatua zitachukuliwa endapo itabainika kuwa madai yao yana ukweli,”
alisema Dk Nchimbi.
Aliwataka viongozi wote wa kisiasa wakiwamo
wa Chadema wanapohisi kutishiwa usalama wao, watoe taarifa polisi ili
vyombo vya dola viyafanyie uchunguzi malalamiko yao ili utaratibu
ufanyike kuhusu usalama wao kama sheria inavyotaka.
Alionya tabia
ya viongozi kuzungumza nje ya utaratibu akisema haikubaliki kwani
inaweza kuwa ni mbinu za kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
Dk
Nchimbi alisema jambo hilo si jema kwani linajenga hofu miongoni mwa
Watanzania na kuwafanya wasiviamini vyombo vyao vinavyowalinda kwa
mujibu wa sheria.
“Ni kweli kuwa kila mwanasiasa anataka kukubalika
na umma lakini, akubalike katika taratibu zinazokubalika,” alisema Dk
Nchimbi na kuongeza:
“Ingekuwa Serikali inataka kukubali umaarufu
kama huo, basi ingetumia mwanya wa haohao Chadema wakati mitandao ya
kijamii iliposambaza taarifa kuwa Chadema ilihusika na kifo cha
marehemu, Chacha Wangwe.”
Alisema Serikali haikukurupuka na
kuwakamata, badala yake ilifanya uchunguzi kwanza na matokeo yake
alikamatwa dereva wake ambaye ameshachukuliwa hatua.
Alisema kama
Serikali ingekuwa inatafuta umaarufu, ilikuwa ni fursa nzuri kwake
kujipatia umaarufu na kukivuruga chama hicho kwa kuwakamata viongozi wa
Chadema hasa baada ya kuwapo kwa uvumi kwamba wamemuua kiongozi huyo.
“Viongozi
wetu wa kisiasa ni lazima wafanye mambo ambayo kesho na keshokutwa
watakiri mchango wao, ama katika ujenzi au uharibifu wa nchi yetu. Kila
siku wakilalamika kuwa wanataka kuuawa basi ni lazima watu watawashangaa
kwani badala ya kutatua matatizo ya wananchi wanabaki wakilalama
wanataka kuuawa. Watu kama hawa wanafanya hivi kwa masilahi yao,
wanaweza kuwagombanisha wananchi.”
Waziri Nchimbi aliwataka
wananchi na viongozi wa kisiasa kuondoa hofu kwani Serikali ina wajibu
wa kuwalinda na hakuna mtu atakayenufaika kwa mauaji ya wanasiasa hao.
Kuhusu
madai kwamba polisi wamekuwa wakipuuza malalamiko ya wapinzani, Dk
Nchimbi alikiri kuwapo kwa baadhi ya polisi wenye kasoro katika utendaji
wao lakini akasema wengi ni waadilifu.
Alisema ikiwa kuna mtu
haridhishwi na utendaji wa polisi kwa kutopata huduma kama
inavyostahili, ana uhuru wa kutoa taarifa katika ngazi za juu hata ikiwa
ni kwake.
Ikulu nayo yatoa tamko
Katika hatua nyingine,
Ikulu imesema hakuna mpango wowote unaoratibiwa na Idara ya Usalama wa
Taifa kwa lengo la kuwaua viongozi hao wa Chadema.
Jana, Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alihoji sababu za Serikali kutaka kuwaua
viongozi hao wakati si tishio lolote kwa nchi.
Balozi Sefue
alisema Idara ya Usalama wa Taifa haiko kwa ajili ya kuua raia au
viongozi, bali kulinda masilahi ya taifa na kuhoji: “Sasa kwa nini
wauawe? Wana nini hasa hadi Idara ya Usalama ifanye hivyo?”
Alisema
ni vyema wakati mwingine kukawa na umakini kwa kuangalia namna siasa
zinavyoweza kufanya kazi... “Hii inaweza kuwa siasa tu. Sisi serikalini
hatuna mambo ya vyama, tunafanya kazi kwa ajili ya watu wote.”
Alisema
Idara ya Usalama wa Taifa na Serikali hazifanyi kazi kisiasa, bali kwa
kuangalia masilahi ya Watanzania wote: “Huku serikalini sisi hatuna
ugomvi na wanasiasa. Tunafanya kazi na watu wote.”
Alisema wanaoweza kufikiria kuwa kuna siasa katika Serikali na vyombo vyake wao ndiyo wanaweza wakawa wanafanya siasa.
Tuhuma za Chadema
Kauli
hizo za Serikali zinatokana na tuhuma za Chadema kwamba kimebaini njama
za kuwaua viongozi wake hao waandamizi ambazo zinaratibiwa na kigogo
mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba nyendo zao zimekuwa
zikifuatiliwa kwa saa 24.
Tuhuma hizo za Chadema zilitolewa juzi
na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Bungeni akisema: “Sisi Chadema hatuna mambo ya siri tunayotaka
kufanya katika nchi hii. Matatizo ya Watanzania yapo wazi na
yanajulikana na kila mmoja, Serikali ya CCM itekeleze sera na ahadi zao
kwa wananchi na si vitisho.”
Neville Meena na Florence Majani, Dodoma- mwananchi
No comments:
Post a Comment