JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana lilimhoji
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi kuhusu
kukaidi amri ya Mahakama iliyotaka wasitishe mgomo.
Juni 22, mwaka
huu, Jaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, Sekela Moshi alitoa amri ya
kusitisha mgomo huo akisema: “Kwa maelezo hayo, ninasitisha mgomo huo
ulioitishwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), hivyo MAT na
wanachama wake hawapaswi kushiriki mgomo huo kama walivyopanga hadi
pande zote mbili zitakaposikilizwa.”
Katibu Mkuu wa MAT, Dk Edwin
Chitega alikaririwa na vyombo vya habari akisema akisema: “Mgomo wetu
hauwezi kuzuiwa na Mahakama, utazuiwa kwa madai yetu kutekelezwa.”
Polisi
kanda hiyo maalumu ya Dar es Salaam, ilithibitisha kumhoji Dk Mkopi
jana na Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Ahmed Msangi alisema
kiongozi huyo alifika Kituo cha Kati cha Polisi kuhojiwa na kisha
aliondoka.
“Ni kweli amekuja mwenyewe. Tumechukua maelezo yake na ameshaondoka,” alisema Msangi.
Akizungumzia
suala hilo, Chitage alisema mwenyekiti wake alitumiwa taarifa ya
kutakiwa katika Kituo hicho cha Polisi Kati kwa simu kutoa maelezo juu
ya madai ya kukaidi kutekeleza amri ya Mahakama iliyotolewa Juni 22,
mwaka huu ikiitaka MAT kusitisha mgomo ulioanza Juni 23, mwaka huu
nchini kote... “Alinipigia simu na kunieleza kuwa yupo huko tangu saa
5.00 asubuhi.”
Amri ya Mahakama
Mahakama hiyo ilitoa amri
kuwataka madaktari hao kuendelea na kazi hadi madai yao ya msingi katika
mgogoro huo yatakaposikilizwa.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Moshi
alisema zuio hilo ni la muda na linalenga kupata fursa ya kusikiliza
kwanza maombi ya msingi kuhusu mgogoro huo.
Katika hukumu hiyo
iliyosomwa bila wawakilishi wa MAT, Jaji Moshi alipanga siku ya
kusikiliza maombi hayo ya msingi na kueleza kuwa hukumu itakayotolewa,
itafungua ukurasa mpya kuhusu mgogoro huo.
Mapema kabla ya amri
hiyo ya Mahakama kutolewa, madaktari walisisitiza kutekeleza azma yao ya
kugoma kwa kubandika matangazo ya kuhamasishana kwenye kuta za
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi).
MAT waomba ulinzi UN
Katika
hatua nyingine, MAT imetoa tamko jipya jana ikiomba Umoja wa
Mataifa(UN), kumwekea ulinzi Dk Steven Ulimboka katika hospitali aliyoko
baada ya taarifa kueleza kuwa kuna timu ya wauaji imetua nchini Afrika
Kusini kuhakikisha harudi nyumbani akiwa hai.
Tamko hilo lilitolewa jana na Dk Mkopi ambaye aliomba pia UN iwawekee ulinzi wadau wote wanaohusika katika masuala hayo.
“Tunataka
pia, Mahakama ishauriwe kuacha kutumiwa kwa faida ya siasa na Bunge
libaki na kazi ya kuhakikisha linaisimamia Serikali kutokana na vifo na
mateso wanayopata watu kutokana na mgomo unaoendelea,” alisema Dk Mkopi.
Hata hivyo, alisema wanakaribisha mawazo kutoka kwa mashirika ya kimataifa ya jinsi gani wanaweza kutatua tatizo lililopo.
Wizara yakata posho
Wakati
huohuo; Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesitisha posho za madaktari
waliokuwa mafunzoni ambao wamegoma hadi hapo itakapopata taarifa ya
uchunguzi wa Baraza la Madaktari.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo
jana na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, Regina Kikuli ilisema posho za
madaktari hao waliogoma zimesitishwa rasmi kuanzia Julai Mosi, mwaka huu
hadi uchunguzi wa Baraza la Madaktari utakapokamilika.
Taarifa
hiyo ilisema wizara hiyo ilipokea malalamiko kuwa kati ya Juni 23 hadi
Juni 29, mwaka huu madaktari 372 walio katika mafunzo kwa vitendo kati
ya 763 katika hospitali mbalimbali nchini, waligoma kutoa huduma kwa
wagonjwa kinyume cha wajibu wao.
Ilisema kitendo hicho siyo tu
kilihatarisha usalama wa wagonjwa waliohitaji huduma za matibabu katika
hospitali hizo, bali kilikuwa ni ukiukwaji wa maadili ya taaluma.
Sehemu
ya taarifa hiyo iliongeza kwamba, hivi sasa madaktari hao hawako maeneo
yao ya kazi na suala hilo limepelekwa Baraza la Madaktari kwa uchunguzi
kuhusu kitendo walichokifanya.
“Kwa kuwa wizara ndiyo yenye
dhamana ya usimamizi wa huduma za afya nchini na kwa kuwa madaktari hao
wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika, hivyo wizara
imewasilisha malalamiko haya huko ili liwachunguze na kuamua hatima yao
kitaaluma,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:
“Wizara inasitisha posho zao kuanzia Julai Mosi, 2012 hadi hapo itakapopata taarifa ya uchunguzi wa Baraza la Madaktari.”
Kuhusu
madaktari wengine waliogoma, taarifa hiyo ilisema taratibu za
kiutumishi zitachukuliwa na mamlaka ya ajira zao kwa mujibu wa sheria na
taratibu husika.
Madaktari hao waliokuwa katika mafunzo ya
vitendo waliogoma, walirejeshwa wizarani kwa barua kutoka kwenye mamlaka
za hospitali walikokuwa wakifanyia mafunzo kwa vitendo.
Wakati
wizara ikisimamisha posho za madaktari hao waliokuwa mafunzoni kwa
kugoma kutoa huduma, Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), imesema kuwa, huduma za afya hospitalini hapo zimerejea katika
hali ya kawaida.
Taarifa ya bodi hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti
wake, Profesa Joseph Kuzilwa iliyotolewa jana kwa umma ilisema kwa
mujibu wa tathmini yake iliyofanyika Julai 7, mwaka huu madaktari wote
waliorejea kazini wanaendelea na kazi kama kawaida.
“Bodi ya
wadhamini imetathmini pia mahudhurio ya madaktari na kuona kwamba wakuu
wa idara, madaktari bingwa, madaktari (medical officers) madaktari
wasaidizi (Asistance medical officers) na madaktari walioko mafunzoni
(interns) wanaendelea na kazi kama kawaida,” ilifafanua sehemu ya
taarifa hiyo.
Boniface Meena, Geofrey Nyang'oro na James Magai
No comments:
Post a Comment